Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wataka kupunguza uagizaji bidhaa kutoka China

Wafanyabiashara wataka kupunguza uagizaji bidhaa kutoka China

Mon, 28 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Uwepo wa viwanda vingi nchini vinavyozalisha bidhaa zenye ubora, utapunguza safari za Watanzania kwenda China kufuata bidhaa hizo.

Hayo yameelezwa na wajasiriamali 10 waliohudhuria kongamano la biashara nchini China chini ya ufadhili wa Benki ya NMB.

Wajasiriamali hao wameeleza kuwa katika ziara hiyo wamebaini China ina viwanda vidogo vidogo vingi ambavyo ndivyo vinazalisha bidhaa wanazotumia gharama kubwa kuzifuata au kuagiza.

Mmoja wa wajasiriamali hao Arnod Mapunda anayejihusisha na uuzaji vifaa vya pikipiki amesema kinachowagharimu Watanzania ni bidhaa nyingi kununuliwa nje ya nchi.

Amesema ziara hiyo imemuwezesha kutambua kuwa inawezekana kuanzisha kiwanda kidogo na ukapata matokeo makubwa.

“Vyote tulivyooona huko vinawezekana endapo tutaamua na hili walione wenzetu wenye taasisi za fedha, wawakopeshe wajasiriamali ili waweze kufanya uwekezaji, tupunguze kuagiza kutoka nje,” amesema Mapunda.

Pia Soma

Advertisement
Naye mfanyabiashara wa maziwa mkoani Morogoro, Rehema Mmari amesema kupitia ziara hiyo ameweza kupata mawazo kadhaa ya biashara ambazo anaweza kuzifanya akipata fedha za kutosha.

Amesema, “Nimefikiria biashara ya nywele maana nimeona mashine ya kutengeneza na vitu vingine vingi vizuri, hakuna sababu ya kununua mzigo nje ya nchi tukiwa na viwanda vidogo hapa nyumbani tunaweza kabisa,”

Kwa upande wake mkuu wa biashara wa NMB, Donatus Richard amesema waliamua kuwawezesha wafanyabishara hao kuhudhuria kongamano hilo ili wakajifunze kutoka kwa wafanyabishara wa China namna wanavyoendesha biashara zao.

Sanjari na hilo ziara hiyo ililenga kujifunza ni namna gani wanaweza kufanya uwekezaji wenye tija hapa nchini ili kupunguza safari za kwenda China.

“NMB huwa tuna klabu za wajasiriamali tunawafundisha masuala mbalimbali ya biashara, mwaka huu tukaona twende mbele tukawapeleka China wakajifunze zaidi kwa kujionea.”

“Wametembelea viwanda na kuhudhuria kongamano la biashara, ni matumaini yetu wamejifunza vingi na watafundisha wenzao kile walichojifunza, maana wametoka katika mikoa ya kanda zote nane,” amesema Richard.

Ziara hiyo ya siku 10 ilianza Oktoba 13 na kuhitimishwa Oktoba 23 wakipata fursa ya kutembelea viwanda vidogo nchini humo.

Chanzo: mwananchi.co.tz