Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara waonywa ulanguzi wa sukari

SUKARI Wafanyabiashara waonywa ulanguzi wa sukari

Mon, 27 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAFANYABIASHARA wa rejareja waonywa kutotengeneza mazingira ya kulangua, kupandisha bei, kwenda kinyume cha bei elekezi ya kuuza sukari.

Wamepewa angalizo kuwa kufanya hivyo kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani, na hatua kali itachukuliwa dhidi yao.

Angalizo hilo lilitolewa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, alipofanya ziara ya kushtukiza ya kukagua sukari iliyopo kama itakidhi mahitaji kwa wakala wa kusambaza sukari Kanda ya Ziwa, V.H. Shah.

Mongella alisema sukari kwa mkoa huo ipo ya kutosha, lakini kuna watu wanaotaka kupandisha bei kwa maslahi yao, hivyo watambue atakayekamatwa kwa kukiuka maelekezo hayo, atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Mawakala wanauza kwa bei elekezi, changamoto ni huko vichochoroni, kuna watu wanapandisha bei hatutaki wakati huu wenzetu wapo katika kipindi cha Ramadhani tunawaletea vikwanzo kwa kupandisha bei sukari,” alisema Mongella na kuendelea: “Na wananchi wanatakiwa kupata mahitaji yao ya msingi wote kwa gharama nafuu bila tatizo.”

Aliongeza kuwa ukaguzi wa bidhaa hiyo ni endelevu na kuwatahadharisha wafanyabiashara hao kuzingatia taratibu, miongozo iliyotolewa.

Pia aliwatakia Waislamu wote mfungo mwema na wachukue taadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID -19 kwa kujikinga na kuwakinga wengine sambamba na kuomba Mungu aliondoe janga hilo.

Naye wakala na msambazaji wa bidhaa hiyo, Pravin Shah, alisema wanazingatia maelekezo waliyopewa ya kuuza kwa bei elekezi, hivyo wananchi wasiwe na hofu sukari ipo nyingi na itakayokidhi mahitaji yao pasipo shaka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live