Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara waomba uboreshaji ulipaji kodi

Jiji Wafanyabiashara waomba uboreshaji ulipaji kodi

Fri, 21 May 2021 Chanzo: ippmedia.com

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao wa masoko ya Sido na  Mwanjelwa walisema kwa sasa hali ya biashara imeanza kuimarika tofauti na ilivyokuwa awali ambapo ubabe ulikuwa unatumika kwenye ukusanyaji wa kodi hali iliyokuwa inawalazimu baadhi kufunga biashara zao.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Atupele Mwinuka alisema tangu  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipotoa  maelekezo wa Mamlaka ya Mapato (TRA) akiitaka kuboresha mazingira kwa wawekezaji na wafanyabiashara hali imeanza kuwa nzuri.

Alisema tangu maelekezo hayo yalipotolewa, maofisa wa TRA wamebadilika na hakuna unyanyasaji tena kwa wafanyabiashara na kwamba hata lugha inayotumika kwa sasa ni rafiki kwao na inahamasisha kulipa kodi.

“Tulikuwa tukiwaona maofisa wa TRA tunafunga biashara na kukimbia, na ilikuwa inasababisha ukwepaji mkubwa wa kodi, walikuwa wakifika Mwanjelwa wenzetu wanatuambia kwamba wameshafika hivyo mjiandae, lakini sasa hivi hata wakikukuta hakuna shida, kilichobakia sasa hivi ni ukadiriaji wa kodi ndio unatakiwa kuboreshwa,” alisema Mwinuka.

Naye Sajo Mwambipile alisema kuna utitili wa kodi ambao pia wanaiomba serikali izipunguze na kuongeza walipa kodi ili kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara wanajiita ni machinga lakini uhalisia unaonyesha kuwa watu hao sio machinga bali ni wafanyabiashara wanaostahili kulipa kodi kama walivyo wengine.

“Serikali ingefanya mpango wa kuhakiki upya biashara ili walipakodi tuwe wengi na viwango vipunguwe, sasa hivi kuna watu wanajificha kwenye mwamvuli wa machinga, lakini biashara ziko vizuri kwa sasa hatukutani tena na vitisho vya maofisa wa TRA,” alisema Mwambipile.

Hata hivyo, alisema biashara nyingi zimeyumba kutokana na mlipuko wa Virusi vya Corona na hivyo ni vizuri Serikali ikaangalia namna ya kuwapa nafuu zaidi wafanyabiashara kwenye ulipaji wa kodi.

 

Chanzo: ippmedia.com