Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara walia utitiri wa tozo, TRA yawatuliza

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga wameeleza kero mbalimbali wanazokumbana nazo na kuiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzifanyia kazi.

Wameeleza hayo leo Ijumaa Julai 26, 2019 katika mkutano kati yao na naibu kamishna wa mamlaka hiyo, Msafiri Mbibo uliolenga kupokea kero na kutoa elimu ya mlipakodi.

Moja kati ya kero zilizotajwa na wafanyabiashara hao ni utitiri wa tozo, zikiwemo za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), zimamoto na mazingira na afya.

“Ukiwa na duka utafuatwa na maafisa wa Halmashauri kutaka leseni ya biashara, watakuja mabwana afya kuhoji kama umelipia tozo ya takataka, akitoka huyo kama ni kiwanda atakuja mtu wa Osha kudai malipo yake.”

“Kabla hujatulia atakuja askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kudai kodi ya zimamoto. Kwanini tozo hizo zisiunganishwe moja kwa moja TRA,” amehoji  Abdallah Kihiyo.

Tozo iliyotajw ana wafanyabiashara wengi na kumlazimu mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella kuwaunga mkono ni ya hoteli na nyumba za kulala wageni, ambapo wafanyabiashara hao walisema inatozwa hata katika hoteli ndogo, badala ya hoteli za kitalii.

Pia Soma

“Unakuta kwenye hoteli zetu za mitaani tunatozwa kodi ya kulaza watalii wakati hawafiki huku. Tumelalamika sana tukaelezwa  itafanyiwa marekebisho lakini bado TRA inatuletea notisi za kutaka tulipe hii ni haki kweli,” amesema  Christopher Haule mmiliki wa hoteli ya Mtendele.

Shigella amesema tatizo ni kiwango cha tozo ambapo hoteli inayotoza mgeni kwa malipo ya dola 150,000 hadi 300,000 tozo yake ni sawa na ya nyumba ya kulala wageni ya Sh10,000 kwa siku.

“Kwa vyovyote vile mwenye nyumba ya kulala wageni anaumizwa kutozwa tozo sawa na mwenye hoteli ya kitalii,” amesema Shigella.

Kero nyingine iliyotolewa katika mkutano huo ni kufutika kwa maandishi kwenye risiti za mashine za kielektroniki za EFD.

Kuhusu leseni za udereva, wafanyabiashara wameitaka TRA Kujipanga kutoa kadi za leseni za madereva ili kuepuka usumbufu wanaoupata wawapo barabarani.

Wafanyabiashara hao pia wameitaka TRA kuondoa vikwazo vinavyosababisha mizigo kuchelewa katika bandari ya Tanga pamoja na mpaka wa Horohoro kutokana na baadhi ya nyaraka kutakiwa kutolewa Dar es salaam.

Kwa upande wake Mbibo amesema TRA ipo katika mazungumzo na Serikali kuondoa baadhi ya tozo ambazo zinaonekana kuwa ni kikwazo kwa wafanyabiashara na nyingine kuunganishwa ili ziweze kutozwa na mamlaka hiyo.

Kuhusu tozo ya hoteli ameahidi kumkumbusha Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla kutekeleza ahadi yake aliyowahi kutoa kwamba anashughulikia.

Chanzo: mwananchi.co.tz