Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wakubwa madini wataja kero 4 

47c00b73bc6c59488f0307da329c9484.jpeg Wafanyabiashara wakubwa madini wataja kero 4 

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA Cha Wafanyabiashara Wakubwa Wanunuzi na Wauzaji Madini Tanzania (TAMIDA) kimewasilisha mapendekezo manne kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philipo Mpango ili kuboresha biashara katika sekta hiyo.

Wakati wa hotuba ya kuaga mwaka 2020 na kuukaribisha mwaka mpya, Waziri Mpango alitoa miezi miwili kwa wafanyabiashara wawasilishe changamoto kwake ili serikali izifanyie kazi.

Mwenyekiti wa TAMIDA, Sammy Mollel alisema jijini Arusha kuwa changamoto katika sekta hiyo ziko nyingi lakini kero ambazo serikali inapaswa kuzifanyia kazi ni pamoja na urasimu katika kuingiza vifaa vya kuongezea thamani madini.

Mollel aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, wafanyabiashara wakubwa wanaonunua madini na kuuza nje ya nchi wanafanya jitihada kuongeza thamani madini hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuagiza mashine za kutosha za kukata madini na kusanifu lakini watendaji bandarini, mipakani na viwanja vya ndege bado ni tatizo.

Kodi ya ushuru wa forodha ya asilimia 25 iliyoondolewa na serikali bado ni kikwazo kwani watendaji wa serikali katika maeneo hayo wanaikwamisha serikali kwa madai kuwa hawana maagizo ya kimaandishi kuondolewa kwa kodi hiyo.

Mollel alisema serikali iliondoa kodi hiyo wakati wa kikao cha Bunge la bajeti lakini kuna urasimu katika utekelezaji wake.

Alidai kuna masharti mapya yamejitokeza katika kuingiza mashine hizo na vifaa vingine vya kuongeza thamani madini nchini, hivyo chama hicho kinamwomba Dk Mpango afuatiliae suala hilo.

Alitaja kero nyingine kuwa ni pamoja na kodi ya zaidi ya asilimia moja ya Wakala wa Meli Tanzania(TASAC) unapotaka kusafirisha madini nje kupitia bandarini.

Mollel alisema wafanyabishara hawagomi kulipa kodi hiyo ila kuna urasimu katika ulipaji kwani kodi hiyo inapaswa kuwepo katika soko la madini kama taasisi zingine ili kurahisisha ulipaji kodi.

Alisema mfanyabiashara mkubwa analipa kila kitu ndani ya soko la madini lililotengwa na serikali ili aweze kusafirisha madini nje lakini kodi ya TASAC haipo katika soko la madini na kufanya mfanyabiashara kwenda tena jijini Dar es Salaam kusubiri kwa muda ili kulipa tozo.

“Tunamwomba Waziri Mpango aingilie kati sula hilo maana linaleta usumbufu mkubwa katika kusafirisha madini nje na linakatisha tamaa wafanyabiashara kufanya biashara ya kusafirisha madini nje na serikali inakosa mapato kwa urasimu uliopo bandarini,”alisema.

Mollel alisema kero nyingine ni kwa namba ya mlipakodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa wafanyabiashara wa madini kulazimishwa kuhamishiwa katika mkoa mwingine bila ridhaa ya mlipakodi.

Alisema TAMIDA ilifuatilia hilo kwa kina kwa viongozi wa TRA Arusha na Mkoa wa Manyara lakini hakukuwa na majibu ya msingi, badala yake viongozi wa mikoa hiyo husema ni maagizo kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu.

Kero nyingine iliyosemwa na TAMIDA ni pamoja na tozo ya Maendeleo ya Elimu ya Ufundi (SDL) ambayo anakatwa mchimbaji katika mshahara wake Sh 400,000.

Mollel alisema kodi hiyo anakatwa mchimbaji bila sababu hivyo chama kinaomba serikali kuiondoa kwa kuwa haiendani na uhalisia wa mlipaji.

Katika kikao cha Januari 22 mwaka jana kilichofanyika Dar es Salaam kati ya wafanyabiashara wakubwa wa madini na Rais John Magufuli, wafanyabiashara walieleza kero zinazowakabili ikiwemo kodi ya ongezeko la thamani(VAT) na kodi nyingine sumbufu rais aliiondoa kodi hizo kwa maslahi ya pande zote.

Chanzo: www.habarileo.co.tz