Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wafunguka chanzo kutojisajili Brela

Brela Wafanyabiashara Wafanyabiashara wafunguka chanzo kutojisajili Brela

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wafanyabiashara wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wametaja kuingiliana kwa nembo za biashara sokoni, mrorongo mrefu wa kupata huduma ya usajili, kuingiliana kimajukumu na kiutendaji baina ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa vikwazo vinavyowafanya kutosajili biashara zao.

Wakizungumza Novemba 15, 2023 katika semina ya kuwajengea uelewa wa hatua za kufanya usajili wa alama za biashara, huduma na hataza kwa njia ya mtandao, wafanyabiashara hao wadogo na kati wametaja changamoto nyingine ni ukosefu wa elimu na ukosefu wa ofisi za Brela ngazi ya wilaya.

“Ofisi za Brela zamani zilikuwepo, baadaye zikatolewa lakini hivi sasa teknolojia ni nyingi na matatizo ya kimitandao ni mengi kwa sababu kuna watu wanatumia fursa hiyo kuweza kutapeli watu.

“Kuna haja kila Mkoa au Wilaya nchini wakawepo mawakala au ofisi za Brela kwa lengo la kuongeza thamani, kuwarahisishia wafanyabiashara kufanya usajili ambapo kwa pamoja utasaidia kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza changamoto hizo za wafanyabiashara," amesema Rashid Bashite, Katibu wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Wilaya ya Misungwi

Katibu Msaidizi wa Mtandao wa Wanawake Wanaojishughulisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA), Fatuma Katulla ameiomba Brela kuzidi kutoa elimu zaidi kwa wananchi na wafanyabiashara ili kila mtu awe na uelewa wa kutosha kuhusu usajili biashara.

"Changamoto ambazo tunazipata kwanza ni kuingiliana kwa nembo unakuta nembo hiyo hiyo inatumiwa na watu zaidi ya mmoja sasa unakuta bidhaa zinaleta shida mtu anahitaji bidhaa ya mtu fulani anaikosa kwa sababu ya nembo zinafanana na hazijasajiliwa," amesema Fatuma

Akizungumzia mafunzo hayo na changamoto hizo Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Hataza Brela, Neema Kitala amesema taasisi hiyo imejipanga kutoa elimu ya usajili na urasilimishaji wa biashara katika mikoa yote nchini.

"Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni wadau wetu kuomba ofisi za Brela ziwe katika kila mkoa au wilaya kwani kwa sasa ofisi zetu zipo Dar es Salaam na Dodoma kwahiyo hatuna ofisi katika mikoa mingine

“Hivyo wadau wameshauri tuanzishe ili kuwasaidia kupata huduma kwa karibu zaidi kwahiyo tumelipokea na tutalipeleka kama ombi kutoka kwa wadau wetu ili kuanzishwa ofisi za kanda au ikiwezekana katika kila mkoa,"amesema Kitala

Chanzo: www.tanzaniaweb.live