Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara waeleza walivyocheka, kulia Krismasi

33327 Pic+krismass Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mikoani. Wakati baadhi ya miji mikubwa wafanyabiashara wakilia kudorora kwa biashara zao katika maandalizi ya Sikukuu ya Krismasi, wenzao wa Dar es Salaam na Mwanza wamechekelea neema.

Wakitoa maoni yao kuhusu sikukuu hiyo, baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wa mikoa mbalimbali nchini walipohojiwa na waandishi wetu, wapo waliosema walisema ukata umewafanya kujikita kwenye ununuzi wa vitu vya lazima zaidi huku wengine wakisema hali ilikuwa nzuri kulinganisha na miaka ya nyuma.

Mmoja wa wachuuzi anayefanya biashara zake Kariakoo, Dar es Salaam, Ali Sultan alisema sikukuu hii ilikuwa neema kwake.

“Hapa nauza viatu kama unavyojionea kwa kweli Krismasi imekuja vizuri watu wananunua kwa wingi, bei ni kulingana na maisha ya Mtanzania ndio maana Watanzania wanahangaika na wanyonge wenzao,” alisema.

Jijini Mwanza, nako kulikuwa na neema, “Hali ya mjini inatisha, watu ni wengi kupita kiasi sijui ingekuwa hivi kila siku pangekuwa panafananaje, yaani inafika hatua inabidi utulie kwanza,” alisema Aneth Shelui mkazi wa Nyamanoro.

Mwingine aliyezungumzia hali hiyo ni Amos Tulope, “Sema tu kwamba huna hela lakini usiseme hatuna hela, watu wana hela bwana, angalia mji ulivyofurika, kwanza inakuwa kero maana hata sehemu ya kukanyaga unakosa, inaonekana kuna watu hata walikuwa hawatoki ndani lakini leo wametoka hii yote ni kwa sababu ya sikukuu.”

Mmoja wa wafanyabiashara wa nguo katika Soko Kuu Mwanza, Mathias Zakaria alisema angalau biashara imekuwa nzuri.

Lakini wakati wafanyabiashara hao wa Dar es Salaam na Mwanza wakichekelea, mfanyabiashara wa viatu katika Soko Kuu Arusha, James Lema alisema tofauti na miaka ya nyuma, mwaka huu biashara imekuwa ngumu mno kwake.

“Nimeleta huu mzigo (viatu) tangu Alhamisi wiki iliyopita lakini nimeuza Sh50,000 tu na thamani ya mzigo ni Sh700,000,” alisema.

Mkazi wa Arusha, Fortunatus Rutta alisema hali imekuwa ngumu kwa kuwa watu wengi hawana fedha.

Hali kama hiyo iliripotiwa mjini Moshi ambako, Edward Riwa ambaye ni mfanyabiashara wa bidhaa mchanganyiko katika Soko Kuu alisema hali ya biashara katika kipindi hiki cha sikukuu kwa mwaka huu haijachangamka kama mwaka jana.

“Krismasi ya mwaka huu ni tofauti na mwaka jana, kwa kuwa watu hawanunui vitu ovyo na ukiangalia maeneo mbalimbali utaona vitu vinavyonunuliwa sana ni chakula lakini vitu kama nguo na bidhaa nyingine utaona watu wanapita tu kuuliza na kuondoka,” alisema.

Pia, muuzaji wa maua na urembo mjini Mtwara, Hassan Juma alisema biashara ya mwaka huu imekuwa ngumu tofauti na mwaka jana.

“Biashara iliyokuwapo msimu wa kuelekea Krismasi mwaka jana sio sawa na mwaka huu, hata ya mwaka juzi ilikuwa na unafuu sana, sasa hivi tukiagiza bidhaa kutoka Dar es Salaam kidogo bei iko juu na ukija Mtwara wateja wale wa miaka ya nyuma hawapo, kwa hiyo kidogo hali ni ngumu,” alisema Juma.

Mchuuzi wa viungo vya chakula Soko Kuu la Mtwara, Issa Chujumba alisema kwa sasa biashara imekuwa ya kawaida na haina tofauti na siku ambazo hazikuwa za sikukuu.

Imeandikwa na Elizabeth Edward (Dar), Mussa Juma (Arusha), Florah Temba (Moshi), Jesse Mikofu (Mwanza), Haika Kimaro (Mtwara) na Godfrey Kahango (Mbeya).



Chanzo: mwananchi.co.tz