Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wadaiwa kero kwa abiria stendi mpya Mbezi

Stend ED Wafanyabiashara wadaiwa kero kwa abiria stendi mpya Mbezi

Sat, 17 Apr 2021 Chanzo: ippmedia.com

Februari 24, mwaka huu Hayati Rais John Magufuli wakati akizindua kituo hicho, alitoa ruhusa kwa wafanyabiashara wadogo kufanya shughuli zao ndani ya kituo hicho.

Lakini kuruhusiwa kwa wafanyabiashara hao, kumesababisha usumbufu kwa wasafiri, kwamba wanafanya biashara hadi katika maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya wasafiri kupumzika.

Wakizungumza na Nipashe, mmoja wa abiria, Iddy Mushi, alisema kitendo cha wafanyabiashara kujazana katika stendi hiyo kinashusha hadhi ya kituo hicho ambacho katika matengenezo yake kiliigharimu serikali zaidi ya Sh. bilioni 50.

Alisema katika baraza zilizotengwa kwa ajili ya abiria kusimama wakati wakisubiria usafiri, kwa sasa panaonekana kama soko kutokana na msongamano mkubwa wa wafanyabiashara uliopo.

“Ukitazama hili eneo lilivyo sasa hata ile heshima ya stendi imepungua, hivyo tunaiomba serikali ilitazame hili kwa ukaribu iweke utaratibu utakaosaidia kuondoa tatizo hili biashara ifanyike lakini kwa utaratibu maalum,” alisema.

Moja wa mawakala wa mabasi, Hashimu Ally, aliiambia Nipashe kwamba kuna baadhi ya abiria wanalazimika kusubiri usafiri ndani ya magari kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuvamia ghorofa ya pili ambayo ipo maalumu kwa ajili ya wasafiri kupumzika, zilipo ofisi za mawakala wa mabasi.

“Abiria wanapata taabu na wengine wanaona shida hata kufika katika eneo hili hivyo tunauomba uongozi kuangalia njia nyingine mbadala ya kuwapanga hawa wafanyabiashara kwa usahihi kwani wakati mwingine inatuwia ngumu kumtambua abiria,” alisema Ally.

Mkurungenzi wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic, alisema Aprili 19, mwaka huu wafanyabiashara wadogo pamoja na wauza chakula watahamishwa na kupelekwa katika jengo ambalo liko nyuma ya kituo hicho ambalo ujenzi wake unamalizika.

Alisema utaratibu wa kuwahamisha ukikamilika, kutawekwa utaratibu maalumu wa kuhakikisha ni mfanyabiashara gani atakayeruhusiwa kuingia kufanya biashara katika stendi hiyo.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara hao watahamishwa ili kutoa nafasi kwa wamiliki wa mabasi kutumia ofisi zilizopo ndani ya kituo kukatia tiketi na waachane na ofisi za nje.

Chanzo: ippmedia.com