Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wa pamba wanavyofaidika na BBT

Pamba Bodi (600 X 353) Wafanyabiashara wa pamba wanavyofaidika na BBT

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha wanunuzi wa pamba nchini (TCA) kimemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha mradi wa Jenga kesho iliyo Bora (BBT) ambao umeanza kuleta mafanikio makubwa katika zao hilo.

Wanunuzi hao wamesema kuwa kupitia mradi huo, katika msimu wa mwaka huu wa kilimo cha pamba, serikali imewapatia maofisa ugani wanaotokana na mradi huo ambao wamesambazwa vijijini.

Katibu wa Chama hicho Bozi Ogola akizungumza na HabariLeo leo ofisini kwake Bariadi, amesema kuwa maofisa ugani hao wamepelekwa katika vijiji na kata ambazo hazikuwa na watalaamu hao hapo awali.

Ogola ambaye pia ni Meneja wa Kiwanda cha kuchambua Pamba Alliance Ginnery amesema kuwa kuletwa kwa maofisa ugani hao kumeanza kuleta tija, kwani wakulima wanafundishwa kilimo bora na mashamba yao kukaguliwa mara kwa mara.

“Kama wanunuzi tunamshukuru sana Rais Samia, moja ya changamoto kubwa kwenye kilimo cha pamba na kuchangia zao kuporomoka ni huduma za ugani, tunaishukuru sana serikali kwa wazo hili, sasa tunakwenda kuongeza uzalishaji na mkulima atanufaika na pamba” amesema Ogola.

Amebainisha kuwa kupitia maafisa ugani hao tangu wamefika vijijini, wametembelea wakulima wengi na kuanza kuwaelekeza jinsi ya kuandaa mashamba, jinsi ya kupulizia sumu, pamoja na namna bora ya kuhifadhi mazao yao.

Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Bariadi na Itilima, Saidi Itaso akizungumzia maofisa ugani hao, amesema kuwa serikali kupitia mradi wake wa BBT iliamua kupeleka watalaamu hao katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live