Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wa mazao watoa kilio chao kwa serikali

624e96f9913252be7f8776944e817e6a Wafanyabiashara wa mazao watoa kilio chao kwa serikali

Mon, 15 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAFANYABIASHARA wa mazao ya nafaka, wameiomba serikali kuweka mazingira wezeshi yatakayowezesha kufanya biashara nje ya nchi bila vikwazo.

Nao mabalozi wa Tanzania katika nchi za Kenya, Zambia, Uganda, Rwanda, Misri na Msumbiji, wamewataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa za kuuza nafaka na viungo, matunda katika nchi hizo.

Walisema hayo juzi mjini hapa wakati wa mkutano kati ya Wizara ya Kilimo na wafanyabiashara hao. Mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Kilimo, Dk Adolf Mkenda.

Mfanyabiashara kutoka Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Bakuza Mingina alisema Watanzania wanapenda kuuza bidhaa nje ya nchi, lakini kumekuwa na vikwazo vikubwa.

"Ukienda kufanya biashara inakuwa ni vigumu kwani wanakuja Tanzania wananunua na wanavusha wenyewe,"alisema.

Daniel Medard kutoka Rusumo wilaya ya Ngara mkoani Kagera alisema wamekuwa wakifanya biashara nchini Rwanda, lakini kuna changamoto ya masoko, kwani nchini humo kuna vikundi vinavyonunua mazao kwa wafanyabiashara kutokaTanzania.

"Wenye vikundi hawana mitaji wakichukua bidhaa wanatafuta masoko, wakiuza wanakuja kukulipa fedha zako na bidhaa nyingine tunazopeleka wanakwenda kuziuza nchini Congo" alisema.

Pia alisema kumekuwa na changamoto ya usafirishaji barabarani, ambapo ushuru umekuwa ukitozwa mara mbili mzigo unapotoka na pale unapokwenda.

Pia alisema maofisa vipimo wamekuwa wakiwatoza faini hadi Sh 500,000 kwa maelezo ya kuzidisha vipimo na hawana mizani ya kupima uzito wa magunia na fedha huchukuliwa bila kuwa na maelezo.

"Unapotoka kwenye wilaya moja kwenda wilaya nyingine bei za ushuru ni tofauti mara gunia moja shilingi 2,000 mara shilingi 3,000” alisema.

Mfanyabiashara wa mchele, Sebastian Mushi kutoka Kilombero alisema aliwahi kusafirisha tani 10 za mchele mpaka Namanga, lakini Wakenya walisema kibali hicho hawakitambui.

"Nilirudi Shirika la Viwango (TBS) ilinichukua wiki mbili kupata msaada na ghala la kuweka mzigo nilikodi kwa siku moja nilikuwa nalipia shilingi 50,000, tunaomba hatua za kushughulikia vibali zifupishwe," alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk Christine Ishengoma alisema juhudi zaidi zinahitajika ili kuongeza mavuno na kupata masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo.

Kwa upande wao mabalozi wa Tanzania wakizungumza kwa njia ya video, waliwataka Watanzania kuchangamkia fursa za kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Misri, Ally Mwinyi alisema kuna soko kubwa la nafaka na viungo nchini Misri. Alisema Misri ina mahitaji ya tani milioni moja za soya kwa mwaka na kuna wakati huwa wanahitaji hadi tani milioni tatu kwa mwaka.

Pia kuna mahitaji makubwa ya pilipili manga, karafuu, matunda na mahindi ya njano.

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Paul Meela alisema kuna fursa za masoko kwenye bidhaa za nafaka, matunda na mafuta.

Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Faustine Kasike alisema kuna soko la kuuza mchele na mahindi na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa hiyo.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk John Simbachawene alisema kwenye mpaka wa Namanga pekee, wanaingiza nafaka na bidhaa nyingine nyingi kutoka Tanzania, ambapo katika kipindi cha Julai hadi Novemba ziliingia jumla ya tani 21,165 za mahindi, mchele tani 2,750, mashudu tani 38,754 na maharage zaidi ya tani 2,000.

Alisema bidhaa zinazohitajika sana Kenya ni mahindi, mchele, maharage, ulezi, viazi mviringo na pumba za mchele.

Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ernest Mangu alisema kuna fursa kubwa ya mazao ya nafaka nchini humo, japo mchele mwingi huagizwa kutoka Pakistan ambao huuzwa kwa bei nafuu.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mkenda alisema serikali itafanyia kazi changamoto zote zilizoelezwa na wafanyabiashara hao. Pia aliwataka kuboresha biashara zao, ziwe za viwango vya kimataifa.

Chanzo: habarileo.co.tz