Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wa China kujenga mabweni, visima Dar

Boardingggggggg.jpeg Wafanyabiashara wa China kujenga mabweni, visima Dar

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi husasani wa kike nchini, Chama cha Wafanyabiashara wa Jiangsu nchini Tanzania, kimejitolea kujenga mabweni mawili na kuchimba visima vitano vya majisafi na salama.

Ahadi hiyo imetolewa jana, JUmapili Januari 21, 2024 na Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Tony Zhang alipotoa salamu za umoja huo kwenye sherehe za mwaka mpya zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobras Katambi, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ACTL), Ladislaus Matindi na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Zhang amesema mabweni hayo yatajengwa kwenye shule ya sekondari itakayopendekezwa na uongozi wa mkoa. Pia visima vitano vitachimbwa kusaidia kupunguza kero ya upatikanaji wa majisafi na salama.

Wafanyabiashara hao pia watatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watano kwenda kujiendeleza kielimu kwenye Jimbo la Jiangsu nchini China kwa gharama za chama hicho cha wafanyabiashara.

Amesema huo ni mchango wa wafanyabiashara hao kwa wananchi wa Dar es Salaam ambao wamekuwa wakishirikiana kuendesha biashara.

“Tunafanya biashara zetu jijini hapa, kuna waliowekeza kwenye viwanda, kufanya biashara katikati ya jiji hasa wilayani Ilala. Hivyo, wanachama wameona wao ni sehemu ya jamii ambayo tunashirikiana nayo vyema. Huu ni mwanzo tutaendelea kusaidia jamii tunayoishi nayo,” amesema Zhang.

Kuhusu mazingira ya uwekezaji na biashara, Zhang amesema wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi kutokana na sera na sheria zilizopo nchini kwa sasa.

Amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa mataifa mbalimbali wakiwemo wa China na kwamba, hilo limeendelea kuwa chachu ya ushirikiano miongoni mwa mataifa hayo rafiki duniani.

“Mazingira, sera na sheria kwetu wawekezaji na wafanyabiashara kutoka China ni rafiki kwa sasa. Hakuna usumbufu kama miaka ya nyuma, tunamshukuru sana Rais Samia kwa hilo,” amesema.

Amesema jukumu la wawekezaji na wafanyabiashara ni kufuata taratibu na sheria za Tanzania kama zinavyoagiza.

“Tulipe kodi kama sheria zinavyotuagiza na kufuata taratibu na utamaduni wa nchi. “Tutaendelea kushirikiana kwenye kujenga mataifa yetu kwa masilahi ya wananchi wetu,” amesema Zhang ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Autobot Garage ya Dar es Salaam.

Naibu Waziri Katambi amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China na mataifa mengine duniani kwamba, Tanzania imeendelea kuboresha sheria na sera za uwekezaji ili kuvutia wageni zaidi.

Amesema kumefanyika mabadiliko ya sheria na sera mbalimbali ili kuongeza ufanisi kwenye uendeshaji wa biashara na uwekezaji na mataifa mengine duniani.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ni muda wa vibali vya kazi kutoka miaka mitano hadi minane na gharama zake ambazo ni Dola za Marekani 1,000 (zaidi ya Sh2.4 milioni) huku muombaji akitakiwa kujaza kwa njia ya mtandao ikiwa ni mkakati wa kudhibiti wanaotapeli wageni.

“Mazingira ni bora zaidi kwa sasa, nipo hapa kuwapa uhakika wafanyabiashara kuwa sera na sheria zetu ni rafiki kwao kuja kuwekezaji nchini. Tumeongeza muda wa vibali vya kazi, hakuna tena mgeni kutembea kwenye maofisi kila kitu anamaliza kwenye mtandao na kupata huduma kwa haraka kwa utaratibu na vigezo vilivyopo,” amesema na kuongeza:

“Msitumie tena wala kutapeliwa na vishoka, teknolojia inafanya kazi yake vizuri, ukikwama kabisa fika kwenye ofisi zetu utahudumiwa.”

Kuhusu usalama wa wawekezaji na wafanyabiashara wa kigeni waliopo jijini Dar es Salaam, Kamanda Muliro amesema: “Dar ni salama kabisa, wageni wanafanya kazi bila hofu kwa sababu tumeimarisha ulinzi.

Natambua nina jukumu kubwa la kulinda mali na usalama wa wakazi wa Dar hivyo, tutaendelea kushirikiana.”

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya, Mpogolo.

Mhandisi Matindi amewahakikishia wafanyabiashara hao wa Jiangsu kuwa, ATCL ipo kwa ajili ya kuwahudumia na kwa sasa inafanya safari tatu kwa wiki kwenda China.

Pia, ameeleza muda wowote kuanzia sasa ndege ya kisasa ya mizigo ya ATCL itaanza safari za kwenda China, hivyo milango iko wazi kwa wafanyabiashara hao kuendelea kushirikiana na shirika hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live