Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara soko la Karume wapelekewa wanasaikolojia

Paych Msaikolojia Dkr Zainab Rashid akimuhudumia mteja wake eneo la Ilala

Fri, 28 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu ya wataalam wa ustawi wa jamii na saikolojia kutoka kituo cha elimu, ushauri na msaada wa kisaikolojia kilicho chini ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii imepiga kambi viwanja vya ukumbi wa jiji, Dar es Salaam kutoa huduma ya elimu, ushauri na msaada wa kisaikolojia.

Huduma hiyo inatolewa bure kwa wafanyabiashara wa soko la mchikichini maarufu Karume, hususani; walio katika kundi maalum, ambao ni wahanga wa janga la moto lilitokea Januari 16, mwaka huu.

Mratibu wa kituo hicho cha elimu na ushauri Bi. Rufina Khumbe amesema Taasisi ya Ustawi wa Jamii iliona ni vyema kwenda kutoa huduma hiyo kwa waathirika wa janga hilo ambao wanauhitaji mkubwa kwa wakati huu.

“Taasisi imekuwa ikitoa huduma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha tunastawisha jamii yetu, kwa kutatua changamoto mbalimbali pia kama Taasisi mama chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum tumeguswa, na ni jukumu la kituo chetu cha ushauri kuja kutoa huduma ya elimu hii na ushauri ili wafanyabiashara hawa hasa wenye uhitaji waweze kulipokea hilo na kulikubali kama changamoto” alisema Bi Khumbe.

Bi. Rufina ameongeza kuwa kutokana na janga hilo la moto wengi wao wamekata tamaa ya maisha, kwasababu mali zilizokuwa zinawaingizia kipato na mitaji vimeteketea na moto huku wengine walichukua mikopo ili kukuza na kuanzisha biashara.

"Mali zimeteketea na hawajui wanalipaje hiyo mikopo. Ndio maana Taasisi ikaona ni vyema kuongea na wafanyabiashara hawa ili kuwapa tumaini tena la maisha yao," amesema Bi. Rufina.

Kwa upande wake msaikolojia kutoka Kituo hicho Dkt.Zainabu Rashidi amesema “tunatoa elimu juu ya kujikinga na majanga mbalimbali ikiwa ni pamoja na moto, mafuriko na pia tunatoa elimu ya namna ya kuyakubali na kuishi na majanga na matatizo baada ya kutokea”.

Aidha Dkt. Zainabu amesema watu wengi wanajua wakifika katika banda la Taasisi ya Ustawi wa Jamii (kituo cha elimu shauri na msaada wa kisaikolojia) watapata msaada wa fedha kwa ajili ya mitaji yao ya biashara.

“Jamii yetu haina uelewa juu ya umuhimu wa huduma ya ushauri na msaada wa kisaikolojia kama tiba ya namna ya kupata suluhu ya matatizo yao kwa kuzungumza na wataalam. Jamii haiamini katika ushauri pekee hivyo tuko hapa ili kuondoa hiyo dhana” amesema Bi. Zainabu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye ulemavu soko la Mchikichini (karume), mzee Juma Hamisi amesema anashukuru Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa elimu,ushauri, na msaada wa kisaikolojia.

“Tumepokelewa vizuri tumepata msaada wa ushauri wa kisaikolojia na elimu na tumewasikia, elimu hii inatupa ujasiri na tumejua kuwa janga hili lililotupata sio letu tu bali ni letu sote” amesema mzee Juma na kuongeza:

“Naishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu kwa kusikia sauti yetu na kuja kutupa msaada wa kisaikolojia na ushauri”.

Zaharan Sulemani mfanyabiashara wa leso, soksi na madaftari katika soko hilo ametoa shukrani kwa Taasisi na kusema kuwa elimu hiyo imewapa ujasiri wa kuanza upya.

“Tunashukuru Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa kuja kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisaikolojia kwa wahanga wa janga la moto pia namshukuru mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuweka sisi wamachinga kwenye kundi maalumu chini ya Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwani tunaaini tutapata usaidizi na usimamizi wa karibu zaidi utakaotufaidisha katika biashara tunazofanya”.

Pia Jumanne Kongogo mwenyekiti wa jumuia ya wafanyaniashara sokoni hapo ametoa wito kwa wafanyabiashara wa soko la karume kwenda kupata huduma hiyo ya elimu na ushauri kwenye banda la Taasisi ya Ustawi wa Jamii.

Ameiomba serikali iangalie jinsi itakavyo jenga soko ambalo miundombinu yake itakidhi kwa wafanyabiashara wenye uhitaji maalumu .

Naye mratibu wa huduma za ustawi wa Jamii kutoka Mkoa, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Jiji la Dar es Salaam Bi. Lilian Chilo ametoa wito kwa wafanyabiashara wa soko la mchikichini kujitokeza kupata huduma inayoendelea kutolewa katika uwanja wa ukumbi wa jiji Ilala kwa siku kumi na nne (14) ambapo huduma hiyo ilianzia katika viwanja vya mnazi mmoja.

Taasisi ya Ustawi wa Jamii chini ya Wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inaunga mkono jitihada za Mh. Rais kutambua wamachinga kama kundi maalum, pamoja na makundi mengine katika jamii yetu.

Zaidi kwa kutoa kipaumbele na umuhimu wa pekee kwa makundi haya kupata huduma za Ustawi wa Jamii ili kuinua na kuboresha hali zao maisha na hasa pindi kunapotokea majanga mbali mbali kama hili la moto katika soko la mchikichini karume.

Taasisi ya Ustawi wa Jamii itaendelea kutoa ushauri wa kitaaluma na ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia kwa jamii ya watanzania na makundi maalum kama sehemu ya jukumu lake la kutoa ‘’Ushauri Weledi” katika fani bobezi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live