Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Wafanyabiashara shusheni bidhaa zenu Soko la Ndugai’

0fc229f08478b76db8a455c9a5e89fa8 ‘Wafanyabiashara shusheni bidhaa zenu Soko la Ndugai’

Fri, 26 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

OFISA Masoko wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Jemes Yuna amewataka wafanyabiashara wa viazi, mahindi, ndizi, nanasi, machungwa na matikiti maji, nyanya na matunda kutoka mikoa mingine nchini, kushusha bidhaa zao katika Soko la Kisasa la Job Ndugai kama walivyokubaliana na si katika masoko mengine.

Yuna amesema serikali imewekeza mamilioni ya fedha katika kujenga soko hilo la kisasa, hivyo ni wajibu wa wafanyabiashara wote wanaopeleka bidhaa au mazao jijini humo kutoka katika mikoa mingine, kushusha katika soko hilo na si katika masoko mengine.

“Nawasihi wafanyabishara wote wanaoleta mizigo yao iwe ya viazi, mahindi, ndizi nanasi, machungwa na matikiti maji na nyanya wote hao wanatakiwa kushusha kwenye Soko la Kisasa la Ndugai ambalo limetenga eneo lao la kushushia mizigo hiyo na siyo huku kwenye masoko mengine.”

“Halmashauri ya Jiji la Dodoma haina ugomvi wala mgogoro na wafanyabiashara wowote wanachotakiwa ni kutekeleza wajibu wao kama walivyoelezwa juu ya umuhimu wa kushusha mizigo kutoka mikoani na sivyo vinginevyo” alisema.

Mapema Januari mwaka huu, Halmashauri ya Jiji ilitoa tangazo la kuwataka wafanyabiashara wote wanaoleta mazao na bidhaa kutoka nje ya mkoa huo, kutakiwa kushusha bidhaa hizo kwenye Soko Jipya la Kisasa la Ndugai na sio mahali pengine kutokana na serikali kuwekeza mamilioni ya fedha katika soko hilo kwa ajili ya kutumiwa na wafanyabiashara hao.

Yuna alitoa maelezo hayo baada ya kuwasikia wafanyabiashara wanaopeleka mazao mkoani Dodoma yakiwemo matunda, viazi na ndizi kutishia kugoma kushusha mizigo yao kwenye Soko la Kisasa la Job Ndugai kwa madai kuwa halina wateja.

Wafanyabiashara hao walidai kutokuwa na imani na watumishi wa halmashauri ya jiji, kutokana na tabia yao ya unyanyasaji wanayoifanya ya kuwafungia minyororo magari yao wanayoleta bidhaa yasiyotekeleza agizo la kushusha katika Soko la Ndugai.

Pia kuwatoza faini kubwa pale wanapoyakuta magari hayo yakiwa yanashusha mizigo kwenye maeneo ya masoko yaliyopo ndani ya jiji na kuwasababishia kupata hasara kubwa.

Mwenyekiti wa Kitengo cha Viazi na Ndizi Soko Kuu la Majengo, Tawakali Ngasso alisema wao kamwe hawatashusha mizigo kwenye Soko la Ndugai, badala yake wataendelea kushusha katika Soko la Majengo hadi pale hatua ya makubaliano itakapofikiwa kwa pande zote mbili.

Ngasso alisema kitendo cha kushusha mizigo inayotoka mikoani vikiwemo viazi na ndizi kwenye Soko la Kisasa la Ndugai kinawaletea hasara kutokana na kukosekana kwa wateja, tofauti na ilivyo kwa masoko mengine yaliyopo ambayo yana wateja wanaokwenda kununua kwa jumla na rejareja.

“Pamoja na serikali kuwekeza mamilioni ya fedha kujenga soko hilo la kisasa changamoto kubwa iliyopo halina wateja kama ilivyo kwenye masoko mengine, hivyo wanalazimika kuendelea kushusha kwenye masoko yaliyozoeleka hata kama halmashauri ya jiji itaendelea kuyafunga magari hayo kwa minyororo,” alisema Ngasso.

Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine iliyopo kwenye soko hilo ni hawana imani na watendaji wa halmashauri hiyo kwa sababu wamekuwa wakichukua uamuzi bila kuwashirikisha wafanyabiashara, hatua ambayo inaonekana ya unyanyasaji na kuwanyima kufanya kazi zao kwa uhuru.

Alisema watumishi hao wa halmashauri wa jiji, wamekuwa wakitumia nafasi zao za uongozi bila kuzungumza nao na kuwaelimisha wafanyabiashara wanaoleta mizigo kwa kutumia magari ili kutatua mgogoro baina yao na watumishi hao.

Chanzo: habarileo.co.tz