Dar/mikoani. Wafanyabiashara wamesifu uamuzi wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kutofunga maduka ovyo ya watakaoshindwa kulipa kodi kwa muda na wengine wametaka jambo hilo liwekwe kisheria ili kuwa na ufanisi.
Jana gazeti hili lilichapisha habari ya mahojiano maalumu na mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo ambaye alisema utaratibu wa kufunga maduka ulisitishwa tangu mwisho mwa mwaka jana na hivi sasa ofisa wa mamlaka hiyo hataruhusiwa kufunga biashara ya mtu isipokuwa kwa idhini ya kamishina mkuu.
Kufuatia hatua hiyo, katibu mkuu wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania (JWT), Abdullah Mwinyi amesema uamuzi huo umekuja wakati mwafaka lakini bado kuna malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara kunyanyaswa na maofisa wa TRA.
“Tunafurahia uamuzi huo lakini tungependa kuona jambo hilo likiwekwa kisheria maana wafanyabiashara wana changamoto nyingi, mwaka jana ulitolewa msamaha kodi kila mfanyabiashara alifurahi hivyo ndivyo inapaswa kuwa,” alisema.
Alisema mambo yakiwekwa kisheria kutakuwa na suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazoikabili jumuiya ya wafanyabiashara ndiyo maana mara nyingi JWT imekuwa ikitaka mazungumzo na Serikali.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema uamuzi huo utaboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini na kuvitia uwekezaji.
Habari zinazohusiana na hii
“Uamuzi umekuja wakati muafaka maana kufungwa kwa biashara hakuathiri tu maduka, bali hata ajira za Watanzania,” alisema Simbeye.Julius Kanangira, mfanyabiashara wa soko kuu Arusha alisema wakati mwingine maisha yanakuwa magumu, hivyo kutokulipa kodi sio kigezo TRA kufunga biashara zao.
“Hili lilikuwa ombi letu muda mrefu kutaka maridhiano katika kodi,” alisema.
Castus Julius alisema, tangazo la TRA siyo tu litasababisha kufunguliwa maduka yaliyofungwa bali pia litahamasisha wafanyabiashara kufungua maduka na kuanza kulipa kodi kwa hiyari.
“Tunajua manufaa ya kodi kwa taifa letu lakini inapokuwa kero kubwa ndiyo hapo baadhi yetu walifunga maduka,” alisema
Johson Leringa, ambaye ni mfanyabiashara katika eneo la stendi kuu ya mabasi Moshi, alisema kwa zaidi ya miaka miwili mkoani humo hajasikia TRA ikifunga biashara ya mtu badala yake hufanya ukaguzi wa kawaida na kuwapa elimu juu ya nini cha kufanya.
“Katika eneo letu tangu mwaka juzi hawajafunga duka la mtu na wanachofanya ni kufanya ukaguzi na kutoa elimu wanapofika kwenye biashara yako na kukuta kuna taratibu hujafuata, jambo ambalo ni tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakitumia madalali kufunga biashara za watu,” alisema Leringa.