Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara bidhaa za mbao walalamikia usumbufu

34296 Pic+mbao Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Handeni. Licha ya ufafanuzi ulitotolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), baadhi ya mafundi na wafanyabisahara wa bidhaa za mbao wamesema kuna usumbufu mkubwa kutoka kwa maofisa misitu katika biashara hiyo.

Wakizungumza jana, mafundi katika karakana za Keko, Dar es Salaam walisema wamekuwa wakikabiliana na usumbufu mkubwa wa maofisa misitu na Polisi wanaposafirisha bidhaa zao.

Fundi aliyejitambulisha kwa jina la Juma Jafar alisema ameshakamatwa na maofisa misitu alipokuwa akisafirisha milango kutoka Keko kwenda Chanika.

“Tunachoshangaa tunakamatwa wakati tayari mbao hizi zimeshalipiwa ushuru huko zilikonunuliwa,” alisema Jafari.

Fundi mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema usumbufu unatokana na ukaribu wa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaa ambazo zinatambulika kama mikoa.

“Hapa tupo Keko, ukisafirisha bidhaa za mbao ukifika Ilala unakamatwa unaambiwa umeingia mkoa mwingine unatakiwa uonyeshe risiti ya mzigo, uonyeshe ilikotengenezewa na uonyeshe usajili. Hayo yote unapata wapi? Sisi ni mafundi wadogo hatujasajiliwa,” alisema fundi huyo na kuiomba Serikali kusajili vikundi vyao ili viwe na utambulisho wa kisheria.

Andrew Kaflete anayesimamia mafundi katika moja ya karakana za Keko aliunga mkono malalamiko hayo akisema mbali na maofisa misitu, Jeshi la Polisi nalo linawasumbua.

“Unaponunua mzigo unatakiwa uonyeshe risiti, ukionyesha bado unatakiwa uonyeshe usajili wa ulipotengenezea, mara risiti ya kusafirishia. Kodi za kununua mbao wameshalipa walionunua mbao. Halafu kwa nini Polisi watukamate wakati kuna askari wa misitu?”

Margaret Kamugisha maarufu Mama Ashura, ambaye ni katibu wa kikundi cha Mwanzo Mzito alisema tozo zinazotozwa kwa mafundi na wasafirishaji bidhaa za mbao ziko kisheria.

“Sisi kwenye kikundi chetu tunanunua mbao na kuuza kwa mafundi. Tunalipia usajili wa kikundi Sh260,000 kwa mwaka na kodi tunazokadiriwa na TRA. Lakini kuna wale wanaoleta mbao kutoka misituni nao wana tozo zao,” alisema.

Hivi karibuni, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ilimwomba radhi abiria aliyekamatwa na ofisa misitu wa Wilaya ya Korogwe akisafirisha kitanda.

Katika taarifa yake, TFS imesema alishindwa kutafsiri masharti ya Kanuni ya 13(4) inayokataza mwenye chombo chochote cha usafiri kusafirisha mazao ya misitu ambayo hayana hati ya usafirishaji.

Jana, ofisa wa TFS wilayani Handeni, Majaliwa Maginga alisema ipo miongozo miwili tofauti ya usafirishaji mazao ya misitu kati ya msafirishaji binafsi na mfanyabiashara wa mazao hayo.

Alisema kama mwananchi atanunua kitanda kwa matumizi yake, zipo tozo atatakiwa kulipa ambazo ni tofauti na mfanyabiashara.

“Kama amenunua kitanda anatakiwa kukilipia TFS Sh20,000 na atapewa kibali kibali ambacho hakihusiani na ushuru wa halmshauri. Hapo anaweza kukisafirisha bila kutozwa fedha yoyote.”

Alisema endapo ni gunia la mkaa lenye uzito wa kilo 50 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, atalipia Sh12,000 ambazo pia ni nje ya ushuru wa halmashauri aliyopo.

“Sheria ya Misitu namba 14 ya mwaka 2002, kifungu cha 93 kanuni ya 13(4) ndiyo inakataza chombo chochote cha usafiri kusafirisha mazao ya misitu, hivyo kwa utaratibu huu, kila chombo lazima kikaguliwe kujua anayesafirisha kama ametimiza vigezo,” alisema Maginga.

Mwenyekiti wa kikundi cha wauza vitanda Mkata, Hossein Ayoub alisema hutakiwa kumwelekeza mteja kwenda ofisi za TFS kulipa Sh20,000 na tozo ya halmashauri ya Sh6,000 ili aruhusiwe kusafirisha bidhaa yake. Alisema tatizo lipo kwa walio kwenye mageti ya ushuru.



Chanzo: mwananchi.co.tz