Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara Soko la Shekilango waomba muafaka na Mkurugenzi Ubungo

Wafanyabiashara Soko la Shekilango waomba muafaka na Mkurugenzi Ubungo

Mon, 11 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

ZAIDI ya wafanyabiashara 600 waliopo Soko la Shekilango Jijini Dar es Salaam ambao wamepewa siku 14 na Manispaa ya Ubungo kuondoka sokoni hapo pamoja na kubomoa vibanda vyao wamesema hawapo tayari kuondoka badala yake wanaomba kukutana na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo-

Wafanyabiashara hao wamesema wameshangazwa baada ya kuona tangazo la kutakiwa kuondoka bila kupewa sababu yoyote.

Wakizungumza leo Mei 10, mwaka huu Jijini Dar es Salaam viongozi wa wafanyabiashara wa soko hilo wamesema hawana tatizo lolote na Manispaa ya Ubungo wala Mkurugenzi lakini tatizo lao ni kutoshirikishwa kwenye majadiliano yanayohusu soko hilo wakati nao ni sehemu ya wawekezaji kwani wanatambua ardhi ni mali ya Serikali lakini vibanda vya biashara ni mali za wafanyabiashara wenyewe ambao wamejenga kwa gharama zao.

Viongozi hao wamesema wapo tayari kutekeleza maagizo yote ambayo watapewa lakini ni baada ya kufanyika mazungumzo ya pande zote mbili tofauti na sasa wanaona tu matangazo ya kutakiwa kuondoka eneo hilo la soko.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara hao, David Mrisho, amesema wamepokea tangazo kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ambalo liliwataka kwenda ofisini kwake kusaini mikataba, huku akifafanua kuwa tangazo hilo linawataka wafanyabiashara hao kulipa kodi ya Shilingi 150,000 kwa frem za nje na Shilingi 50,000 Kwa frem za ndani badala ya kodi ya sasa ya shilingi 15000 wanayolipa kwa kila mwezi mbali ya gharama zingine zikiwemo za leseni na ushuru.

"Hizi gharama za kodi ambazo tunatakiwa kulipa ni kubwa sana kwetu sisi wafanyabiara lakini hata mchakato wake wa kupanga tozo hizo hatukushirikishwa ili nasi tuseme uwezo wetu na changamoto tunazozipata. Hivyo sisi tunaendelea kuiomba Manispaa tukae pamoja tujadiliane," amesema Mrisho.

Aidha, Mrisho amesisitiza kuwa kimsingi wao ni sehemu ya wawekezaji katika soko hilo kwasababu vibanda ni mali yetu na ardhi mali ya serikali na wamekuwepo hapo tangu mwaka 1975 na hawana matatizo na mamlaka huku akieleza kuwa wamekuwa wakilipa kila kinachotakiwa na serikali. Sasa wamepewa tangazo la kuambia wasaini mkataba wa pango za frem na mwisho wa kusaini ilikuwa Aprili 23 mwaka huu.

"Lakini cha kushangaza hiyo mikataba ambayo tunatakiwa kusaini hatujawahi kuiona wala kuletewa na sasa tunaambiwa tuondoke ndani ya siku 14 kwa kile walichodai tumekataa kusaini mkataba huo ambao hatujawahi kuuona," amesema Mrisho.

Kwa upande wake Katibu wa soko la Jumuiya ya wafanyabiashara Shekilango Adamu Yusuph amesema kuwa kitendo cha kutaka kuondolewa katika soko hilo bila kufanya mazungumza ni kutaka kwenda kuathiri maisha ya watu zaidi ya 600 ambao nao nyuma yao kuna kundi kubwa la watu wanaowategemea, hivyo ni vyema busara ikatumika ili kupata ufumbuzi sahihi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live