Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Pugu Kajiungeni jijini Dar es Salaam wamemuomba Rais wa Tanzania, John Magufuli kuingilia kati mgogoro katika eneo lao la biashara kwa madai kuwa baadhi ya watendaji wameshindwa kuwasaidia.
Mwaka 2016 eneo hilo lilivunjwa na mtu mmoja aliyedai kuwa ni lake.
Wakizungumza leo Jumapili Septemba 8, 2019 wakati wakigawana upya maeneo ya biashara tayari kuanza ujenzi wa vibanda, wamesema wamechukua uamuzi huo baada ya kukosa msaada wa viongozi serikalini.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Peter Majura amesema tangu walipovunjiwa hawajasikilizwa kwa madai kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakishirikiana na waliovamia eneo hilo.
"Tunamuomba Rais Magufuli kuingilia kati mgogoro huu kwa kuwa tangu tumevunjiwa hakuna mtendaji yoyote aliyefika eneo hili,” amesema Majura.
Amebainisha kuwa watendaji wameshindwa kuwasikiliza akiwemo mwenyekiti wa mtaa huo na badala yake amekuwa akijimilikisha maeneo na kuuza viwanja.
Pia Soma
- Hospitali ya Bugando mbioni kuanzisha taasisi ya moyo
- Mke wa Babu Seya ataka Watanzania kuwaombea maisha mema
- Makonda: Nitawatetea wanawake Dar hata nikichukiwa na wanaume
Diwani wa Pugu, Boniventure Mfuru amesema awali eneo hilo lilikuwa likimilikiwa (anamtaja jina) lakini baadaye aliamua kulikabidhi kwa vijana kwa ajili ya kufanya biashara.
Amesema kila anapoeleza jambo hilo katika vikao vya baraza la madiwani, hujibiwa kuwa mgogoro huo unashughulikiwa.
“Kiwanja hiki ni muhimu kwa maendeleo ya Pugu, wananchi walikaa na kukubaliana kurudi kwenye maeneo yao na mimi nabariki kwa kuwa hatujapata majibu kutoka kwa viongozi,” amesema Mfuru.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bombani, Gido Lupiana amesema eneo hilo lina mgogoro na tayari kesi ipo mahakamani.
"Wiki mbili zilizopita tuliletewa zuio la kutofanya chochote hadi kesi iliyopo mahakamani itakapoisha hata mtendaji alishawaandikia barua,” amesema Lupiana
Amesema Serikali ya mtaa ndio waliowapa eneo hilo kwa maelekezo kuwa endapo atatokea mwenye eneo au Serikali ikilihitaji, wawe tayari kuondoka.