Licha ya serikali kufanyia kazi baadhi ya maoni yaliyowasilishwa na wafanyabiashara katika kamati maalumu iliyoundwa na waziri mkuu kukusanya kero za wafanyabiashara nchini lakini wafanyabiashara mkoani Njombe wanasema bado Kuna changamoto kubwa katika ushuru wa vyombo vya Moto hususani magari ya mizigo na abiria ambao unatozwa sawa kwa gari chakavu na mpya.
Wakizungumzia katika mkutano wa wafanyabiashara hao wakati Kamati hiyo ilipofika kutoa mrejesho wa changamoto zao,Baadhi fanyabiashara mkoani Njombe akiwemo Metord Danda wamesema hali ya biashara ni mbaya mjini Njombe hivyo wanaiomba serikali kuendelea kurekebisha sheria za kodi kwasababu zinawafanya watu kufilisika na kufunga biashara Huku pia wakisema suala la kupunguza faini ya kutokata risiti za EFD kumetazama uhalisia.
“Kwa mazingira ya mwanzo ya sheria ya faini kwa mtu atakaekutwa na kosa la kuuza bidhaa bila kutoa risiti za EFD yalikuwa kandamizi kwasababu mfanyabiashara anakamatwa ameuza chipsi ya elfu tatu bila risiti lakini anapigwa faini ya mil nne na nusu Jambo hili lilikuwa likisababisha watu kufikiria hata kuloga,alisema Onesmo Mwajombe.”
Aidha, wameomba serikali kuitazama changamoto ya TINI kutumika na watu wengine bila ridhaa yao kwa kuziunganisha kwenye mfumo ili Pindi itakapo tumika ujumbe ufike na mfanyabiashara kuchukua hatua haraka.
Awali, Specioza Mickness Owure ambaye ni meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Njombe ambaye ametolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali za kikodi huku akitoa onyo kali kwa wanaofanyakazi ya kuuza risiti mitaani.
Kwa upande wake aliyekuwa Makamu mwenyekiti wa kamati iliyoundwa na waziri mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashra Tanzania Hamis Livembe amesema hivi sasa serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupungza kero za wafanyabiashara tofauti na kipindi kilichopita.
Katika hatua nyingine amewataka wafanyabiashara kuendelea kubainisha changamoto nyingine zinazokwamisha ustawi wa biashara nchini ili waziwasilishe serikali zichukuliwe hatua katika maboresho.
Bado kamati hiyo inaendelea kupita katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kutoa mrejesho wa utatuzi wa kero zao pamoja kuchukua nyingine.