Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara Mwanza wapewa siku 10 kuhama kupisha ujenzi

73030 Pic+mwanza

Mon, 26 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Wafanyabiashara zaidi ya 780 wa soko kuu jijini Mwanza nchini Tanzania wamepewa siku kumi kuanzia leo Jumatatu hadi Septemba 5, 2019 wawe wamehamia soko la muda la Mbugani kupisha ujenzi wa soko jipya la kisasa utakaogharimu zaidi ya Sh23 bilioni.

Amri hiyo imetolewa leo Jumatatu Agosti 26,2019 na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk Philis Nyimbi alipotembelea soko hilo ambapo amesema mpango huo unalenga siyo tu kuipa soko hilo hadhi ya Kimataifa kulingana na hadhi ya jiji, bali pia itatoa fursa kwa wafanyabiashara wengi zaidi kulinganisha na waliopo sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amesema soko jipya linalojengwa litakuwa na jengo la ghorofa mbili lenye vyumba 500 vya biashara na vizimba 1,500 pamoja na eneo la kuegesha magari zaidi ya 500 kwa wakati mmoja.

Soko Kuu la sasa lina vizimba 520, maduka 178, bucha 14 migahawa 21, sehemu za kupanga biashara ya ndani ya soko 47 na maeneo kadhaa ya kupanga biashara nje linalotumiwa na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara Soko Kuu la Mwanza, Ahmad Nchola amesema wako tayari kutekeleza amri hiyo na tayari asilimia 95 ya wafanyabiashara wamesaini mikataba ya kuhama kwa baada ya kuahidiwa kurejea ujenzi utakapokamilika baada ya miezi 24 ijayo.

“Tunaiomba jiji kukamilisha ujenzi wa miundombinu ikiwemo vyoo, uzio, huduma ya maji na umeme ili tutekeleze amri ya Serikali ya kuhama,” amesema Nchola

Pia Soma

Pamoja na soko jipya, jiji la Mwanza pia linatekeleza ujenzi wa maegesho ya magari makubwa eneo la Buhongwa, nje kidogo ya jiji la Mwanza kwa gharama ya Sh13 bilioni.

“Pia tunajenga stendi kuu la kisasa eneo la Nyegezi litakalokuwa na eneo la maegesho ya mabasi na magari mengine pamoja na jengo la ghorofa mbili kwa ajili ya ofisi za makampuni ya mabasi na maeneo ya biashara kwa gharama ya Sh14 bilioni,” amesema Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa jiji.

Miradi hiyo mitatu ya soko jipya, stendi mpya ya mabasi na maegesho ya malori inayogharimu zaidi ya Sh50 bilioni ilitakiwa kuanza Julai Mosi, 2019 lakini imechelewa kutokana na kutokamilika kwa miundombinu kwenye maeneo ambako shughuli za stendi na soko zinakohamishiwa kwa muda.

Wakati wafanyabiashara soko kuu wakihamishiwa soko la Mbugani, stendi kuu ya Nyegezi ilioko mtaa wa Nchenga imehamishiwa kwa muda mtaa wa Nyabulogoya jirani na shule ya sekondari Nyabulohoya.

Uamuzi ulioibua hofu ya kukosekana kwa usikivu nyakati za masomo miongoni mwa wanafunzi na jumuiya ya shule hiyo.

“Sijui vigezo vilivyotumika kuhamishia stendi jirani na shule; lakini uamuzi huu siyo tu utaathiri usikivu na umakini darasani, bali pia maadili na maendeleo kitaaluma," Castory Jonathan mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari Nyabulogoya ameiambia Mwananchi

Gertrude Shimbe, mwanafunzi mwingine wa shule hiyo ameziomba mamlaka husika kuwadhibiti madereva kuepuka vurugu na ajali nyakati za asubuhi na jioni.

Kuhusu hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa jiji, Kiomon Kibamba amesema Serikali imechukua tahadhari kuhusu ulinzi na usalama wa wanafunzi kwa kipindi chote cha miezi 24 stendi ya muda itakapokuwa eneo hilo ikiwemo kujenga uzio eneo lote la shule kudhibiti mwingiliano na vurugu za stendi kwa wanafunzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz