Serikali imesema ipo katika hatua mbalimbali za kuhakikisha kila mfanyabiashara kwenye Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, anarasimishwa ili awe kihalali na atozwe kodi.
Lengo la hatua hiyo, ni kukomesha biashara zisizo rasmi na zisizotozwa kodi katika soko hilo, kadhalika kuondoa utaratibu wa wafanyabiashara wakubwa kuwatumia machinga kukwepa kodi.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam katika kikao cha mawaziri na wafanyabiashara, ili kutatua changamoto za biashara katika soko la Kariakoo zilizowasilishwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mawaziri walioshiriki kikao hicho ni, Dk Mwigulu Nchemba (Fedha), Profesa Kitila Mkumbo (Mipango na Uwekezaji), Dk Ashatu Kijaji (Viwanda na Biashara) pamoja na Daniel Sillo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.
Profesa Kitila amesema kila biashara itarasimishwa sokoni hapo.
Ili kutekeleza hilo, Waziri huyo ameeleza utaratibu wa kisheria unaandaliwa kuhakikisha kila biashara katika soko hilo, inatozwa kodi.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuona kunaibuka fursa mpya za kibiashara zinazofanyika kwa mfumo rasmi.
"Uwekezaji lazima uongezeke, lazima kuwepo na biashara mpya zinazolipa kodi," alisema akisisitiza Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara.
Amesisitiza hakuna namna nyingine ambayo Serikali itaitumia kutanua wigo wa kodi, zaidi ya kuzirasimisha biashara.
Msingi wa hoja ya Profesa Mkumbo ni malalamiko ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Luvembe aliyesema wapo wanaowatumia machinga kukwepa kodi.
Akifafanua hilo, Luvembe amesema wafanyabiashara rasmi katika soko hilo, wanawapa machinga bidhaa zao wawauzie ili kukwepa kodi.
Lakini amesema hayo ni matokeo ya machinga kuruhusiwa kuuza bidhaa zinazofanana na wanazouza wafanyabiashara rasmi, huku wao wakiwa hawalipi kodi.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Martin Mbwana, amelalamikia uwepo wa biashara nyingi ndogondogo za Wachina katika soko hilo.
"Naomba Serikali ihakikishe katika Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki (EABC) Wachina hawamiliki biashara nyingi zaidi ya Watanzania," amesema.
Kuhusu hilo, Profesa Mkumbo amesema ni asilimia tano tu ya maduka ndiyo yatakayomilikiwa na Wachina huku mengine yote yakimilikiwa na Watanzania.
Amesema kituo hicho kitakuwa na maduka zaidi ya 2,000 na eneo la kuhifadhia bidhaa.
Amesema eneo hilo linatarajiwa kuzalisha ajira na mitaji na jambo bora zaidi ni namna Watanzania watakavyonufaika nazo.
"Uwekezaji ni muhimu, lakini lazima tutengeneze sheria kuhakikisha Watanzania wanakuwa zaidi ya wageni. Kati ya maduka, 1,860 yatakayokuwepo katika eneo hilo, 93 ndiyo yawe ya Wachina na yaliyobaki yamilikiwe na Watanzania," amesema.
Alipozungumza katika jukwaa hilo, Waziri Kijaji ameulekeza Wakala wa Usajili wa Biashara (Brela), kuanzisha kliniki za biashara katika soko la Kariakoo ili kuwezesha urasimishaji wa biashara na wawe walipa kodi.
Amesema biashara hazipaswi kufungwa, bali jambo muhimu ni wafanyabiashara kulipwa kodi kama inavyopaswa.
Katika hilo, amesema Brela inapaswa kuhakikisha kila mfanyabiashara anatambuliwa na anaunganishwa katika mfumo wa ulipaji kodi.
Amesema changamoto 21 zilizowasilishwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mwaka jana, 16 zimeshatatuliwa na tano zinaendelea kufanyiwa kazi zikiwemo zile za kikodi.
Kwa upande wake, Waziri Mwigulu amesema Mei 25, mwaka huu atakutana na kikosi kazi ili kufanya mapitio ya masuala yote ya kikodi yanayolalamikiwa.
"Tutakutana na viongozi wa wafanyabiashara kuangalia masuala yanayohusu kodi na kuyashughulikia kwa haraka kwa kuwapeleka bungeni," amesema.