Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara K’koo walia mauzo kiduchu kuelekea Krisimasi

89647 Kkoo+pic Wafanyabiashara K’koo walia mauzo kiduchu kuelekea Krisimasi

Mon, 23 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ikiwa zimesalia siku chache kabla ya Watanzania kuungana na mataifa mengine duniani kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, kilio cha hali ngumu kimetawala kwa wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa zinazotumika katika sikukuu hizo.

Ni kawaida wakati wa kuelekea kwenye sikukuu hizo watu huanza mapema maandalizi kwa kununua mavazi ya watoto pamoja na mapambo ikiwemo maua na miti ya krismasi.

Wafanyabiashara ambao ndio wauzaji wa bidhaa hizo wanasema mwaka huu umekuwa mgumu zaidi kwao kutokana na kukosa wateja licha ya kuuza bidhaa hizo kwa gharama nafuu.

Mwananchi ilitembelea soko la Kariakoo na kushuhudia msongamano mkubwa wa watu wakipita huku na kule kufanya manunuzi huku neema ikionekana kuwa zaidi upande wa wamachinga.

Watu wengi walionekana wakiangalia nguo na viatu vya watoto vilivyopangwa mezani.

Mmoja wa wamachinga hao, Haji Salum alieleza kuwa gharama nafuu imekuwa sababu kwa wanunuzi wengi kuwakimbilia wao badala ya madukani.

“Hapa ukiwa na Sh20,000 una uhakika wa kupata nguo ya juu na chini kwa mtoto, ndiyo maana unaona watu wengi wanachagua kwenye meza lakini bado sioni mwaka huu kama kuna biashara, zamani wakati kama huu kungekuwa hakuna mahali pa kukanyaga.”

Kwa upande wake, Yahya Athumani ambaye ni mchuuzi wa viatu amesema wateja wengi huishia kuulizia bei na kuondoka wanapotajiwa.

Alisema hatua hiyo inawaweka kwenye wakati mgumu ikizingatiwa siku zimebaki chache kabla ya msimu wa sikukuu kumalizika na watu kuingia kwenye majukumu mengine muhimu ikiwemo ada na kodi.

“Ninachoona hali ya uchumi haiko vizuri, maana unaweza kuona wateja wanakuja wengi ila si wote wananunua wapo wanaokuja kuuliza bei ukimtajia anageuza, sasa kwa mtindo huu sijui tutaishi vipi sisi tunaotegemea kuendesha familia kwa biashara za kuungaunga,” alisema.

Maduka vs wamachinga

Akizungumzia hilo, Elias Kilewo ambaye ni mmiliki wa duka la nguo alisema mwaka huu biashara imekuwa ngumu zaidi huku akipeleka lawama zake kwa wamachinga kuwa ndiyo wanawachukua wateja wao.

“Wamachinga wametuharibia biashara, yani wateja hawaingii ndani wote wanaishia huko nje, sisi tunaishia kushangaa tu angalia hakuna watu tuna wakati mgumu mno,” alisema Kilewo na kuongeza.

“Hata bei tumejaribu kushusha ili suala la gharama lisiwe tatizo, sasa hivi suruali za watoto tumeshusha hadi kuanzia Sh12000, miaka iliyopita zilianzia Sh18000 lakini bado watu wanaishia nje kwa wamachinga kununua nguo zisizokuwa na ubora,” alisema.

Naye Bertha Temba alisema mzigo wa nguo za watoto haujauzika kama ambavyo alitarajia na badala yake wateja wanaofika wanaulizia sare za shule na masweta.

“Mwaka huu Kariakoo imekuwa nyeupe, mizigo tunayo lakini hakuna wateja, wanaokuja wanaulizia nguo za shule, wachache wanaoulizia nguo ukimtajia bei anashtuka. Yaani mtu unamwambia suruali Sh15,000 anasema umuuzie 10000 sasa hapo unawezaje ndiyo matokeo yake nguo tumebaki nazo,” alisema Temba.

Miti na mapambo yadoda

Wakati kwenye nguo na viatu kukiwa hivyo upande wa mapambo nako hali si shwari, wachuuzi wa miti na mapambo nao wamelalamika kukosa wateja.

“Nashindwa kuelewa ndiyo hali ngumu ya uchumi au watu bado wana mapambo ya miaka iliyopita. Hatuoni wateja, zamani tarehe kama hizi nimeshachukua mzigo mara mbili lakini mwaka huu nimechukua mara moja na bado upo wa kutosha,” alisema Seleman Alex.

Kwa upande wa Omary Mbunda, aliwasisitizia wateja kuendelea kujitokeza kununua mapambo hayo kwa kuwa yana nafasi kubwa ya kuchangamsha nyumba wakati wa sikukuu.

Kauli za wanunuzi

Ali Nyange, mkazi wa Ubungo alisema hali ngumu ya uchumi imekuwa kikwazo kikubwa kwa watu wenye kipato kidogo kumudu gharama za bidhaa hizo.

“Tunalazimika kwa sababu hatuna namna ya kufanya lazima watoto wavae, ila kiukweli hali ya uchumi sio nzuri wengi wanaangalia mahitaji muhimu na ukizingatia Januari hiyo inakuja moto unakwenda kuwaka zaidi,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz