Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara Ilala Boma walia ushuru wa bidhaa

Fri, 18 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyabiashara katika Soko la Ilala Boma, wamemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati tozo wanayotozwa wanapoingiza bidhaa sokoni hapo.

Akizungumza na Gazeti la Mwananchi, mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Idd Maleta alisema bidhaa zinazolipiwa mlangoni kabla ya kuingizwa sokoni ni za shambani ambazo hutozwa Sh500 kwa tenga moja la nyanya.

Pia, kiroba cha bamia, pilipili na matunda kwa kiroba na mkungu wa ndizi hutozwa Sh500 kwa kila kimoja.

“Kikao cha kujadili kero mbalimbali kilichofanyika Februari 24, mwaka jana, wajumbe waliazimia kuondoa ushuru wa Sh500 kwa kila bidhaa ya shambani inayoingizwa katika soko hili lakini bado unaendelea,” alisema Maleta.

“ Sisi ni wafanyabiashara wadogo, tunaosimamia bidhaa zinazotoka shambani, tunaomba Rais wetu atusaidie ili tuondolewe ushuru huu kwa sababu tunavyotozwa ushuru mara mbili ni pigo kwetu,” alisema Juma Liteleko ambaye ni katibu wa kikao hicho.

Liteleko alisema ushuru huo umekuja baada ya Kampuni ya Mp Environment kupewa zabuni ya kukusanya ushuru katika soko hilo na umekuwa ukipingwa na wafanyabiashara.

Hata hivyo, meneja wa kampuni hiyo, Gamdust Haji alisema wanakusanya ushuru kwa mujibu wa sheria kutokana na makubaliano ya kimkataba baina yao na halmashauri.

“Kwa mwezi tunatakiwa kukusanya Sh167 milioni katika soko la Ilala Boma, niseme tu tozo zote wanazozilalamikia wafanyabiashara hao, zipo kisheria,” alisema Haji.

Naye ofisa wa Soko la Ilala Boma, Selemani Mfinanga alisema kwamba ushuru unaotozwa uko wa aina mbili.

Alifafanua kuwa kuna ushuru wa kuingiza bidhaa na ushuru wa kupanga kwenye vizimba hivyo sintofahamu iliyopo huenda inatokana na kutolijua hilo.

“Ushuru huu unatozwa kwa mujibu wa sheria ndogo za uendeshaji wa soko za halmashauri ya Manispaa ya Ilala za mwaka 2015 ambazo ni sheria halali zilizosainiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa katika Serikali ya awamu ya awamu ya nne, hakuna mtu anayelipa ushuru kinyume cha sheria,” alisema Mfinanga.



Chanzo: mwananchi.co.tz