Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara Geita walia makadirio ya kodi

8d27a1a111102180a581b3ce9419b55a Wafanyabiashara Geita walia makadirio ya kodi

Sun, 10 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAFANYABISHARA katika Halmashauri ya mji mdogo wa Katoro mkoani Geita, wamelalamikia makadirio makubwa ya kodi yanayofanywa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwenye biashara zao.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa mkutano kati ya wafanyabishara hao na uongozi wa TRA mkoani humo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabishara mjini Katoro, Charles Makanji alisema changamoto hiyo imekuwepo kwa muda mrefu.

Makanji alisema makadirio ya kodi yanayofanywa na maofisa wa TRA yamesababisha wafanyabishara wengi kuchelewa au kushindwa kulipa kodi hivyo wanatozwa faini na biashara zinafungwa.

"Makadirio ya kodi ni makubwa mno, hayaendani na biashara zetu, wengi wamefunga maduka, wameamua kufungua vibanda barabarani ili walipie Sh 25, 000 kwa mwaka wapate kitambulisho cha mjasiriamali, maafisa wa TRA nao tukiwafuata wanatoa vitisho, hii ni shida kubwa kwetu," alisema Makanji.

Mfanyabiashara katika mji mdogo wa Katoro, Medadi Gamaya alitoa mfano kuwa mwaka 2016 makadirio ya kodi aliyopatiwa ilikuwa 150,000/- , mwaka 2017 ilikuwa 200,000/-, mwaka 2018 ilikuwa 450,000/- na mwaka 2019 ilikuwa zaidi ya 500,000/-.

Alisema, mwaka 2020 aliletewa makadirio ya kodi ya sh. milioni 4.46 huku mtaji wake ukiwa hauzidi Sh milioni 10; hivyo kusababisha ashindwe kulipa kodi na sasa anafikiria kufunga biashara ama kuhamishia eneo lingine.

Meneja wa TRA Mkoa wa Geita, Hashim Ngoda aliahidi kufanyia kazi malalamiko na kuwaomba wafanyabishara watunze kumbukumbu zao za biashara na risiti za mauzo na manunuzi ili kuwasaidia maofisa wa TRA kujiridhisha kabla ya kufanya makadirio ya kodi.

Chanzo: habarileo.co.tz