Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara, CTI watoa malalamiko mbele ya mawaziri tisa

Wafanyabiashara, CTI watoa malalamiko mbele ya mawaziri tisa

Fri, 6 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam nchini Tanzania wameiomba Serikali kutenga eneo lingine la biashara kutokana na kituo hicho cha biashara kujaa.

Ombi hilo limetolewa leo Ijumaa Desemba 6, 2019 kwenye mkutano wa mashauriano kati ya Serikali, wawekezaji na wafanyabiashara wa mkoa wa Dar es Salaam.

Mawaziri tisa wanashiriki mkutano hio wenye lengo la kushauriana jinsi ya kuvutia uwekezaji na kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuondoa kero zinazokwamisha biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Elias Marwa amesema eneo la Kariakoo kwa sasa limejaa na linahitaji kupumua.

“Soko la Kariakoo limejaa, hakuna hata kwa kukanyaga, tunaomba mtupatie eneo lingine la ekari 20 ili wafanyabiashara wajenge soko jingine kwenye barabara ya Morogoro kabla ya kufika Kibaha,” amesema

Marwa pia amelalamikia utaratibu mbovu uliopo bandarini kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wanaoingiza mizigo kutoka nje ya Tanzania na hata kufikia hatua ya kufilisika.

Amesema katika bandari ya Dar es Salaam yametengenezwa mazingira ya watu kutoa rushwa ili kuruhusu mizigo yao kupita kwa kodi kidogo.

“Pale bandarini shida inaanzia kwenye uthaminishaji yaani mtoza kodi anaamua aseme kiasi gani hapa sasa ndiyo mazingira ya kuzungumza yanapoanzia,” amesema Kamote

Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) Hussen Kamote amesema lengo la kufikia uchumi wa viwanda linaweza lisifikie endapo changamoto zilizopo hazitatafutiwa ufumbuzi.

Ameitaja moja wapo ni kukosekana kwa sera maalum ya kulinda viwanda vya ndani kutokana na bidhaa kutoka nje kuingia kwa wingi nchini na kuuzwa kwa bei nafuu.

 

Changamoto nyingine ni kutotabirika  kwa mfumo wa kodi, kila mwaka serikali inakuja kodi mpya jambo linalowafanya wenye viwanda kushindwa kujipanga.

 

Mawaziri wanaoshiriki mkutano ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angella Kairuki; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

 

Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni;  Naibu Waziri wa Madini, Stanislaus Nyongo; Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu; Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega;  Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Antony Mavunde na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya.

Chanzo: mwananchi.co.tz