WAFANYABIASHARA zaidi ya 300 kutoka mkoa wa Mwanza wamenufaika na elimu ya mikopo kutoka benki ya NMB.
Akizungumza wakati wa kongamano la siku ya jukwaa la klabu ya biashara iliofanyika Agosti 17, 2023 katika ukumbi wa Rock City, Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Ziwa, Dickson Richard amesema wametoa elimu hiyo ya kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu uchukuaji na urejeshaji wa mikopo.
‘’Nawashukuru sana wafanyabiashara ya benki yetu haswa kutoka Mkoa wa Mwanza mmekuwa mstari wa mbele katika uchukuaji wa mikopo na mmekuwa mnarejesha kwa wakati’’ amesema Richard.
Amesema kupitia jukwaa hilo wameweza kufundisha elimu ya kodi, utafutaji wa masoko pamoja na upangaji wa bei ya bidhaa. Amesema kupitia jukwaa hilo wamefaidika kwa kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara.
Amewaomba wafanyabiashara kuendelea kutumia huduma ya kibenki kwa mtandao ili wafanyabiashara waweze kupata wateja zaidi.
‘’Kupitia huduma yetu ya NMB mkononi, mfanyabiashara anaweza kupata mkopo wa haraka mpaka Sh 500,000’’ amesema Richard.
Mwenyekiti wa klabu ya biashara ya benki ya NMB Mkoa wa Mwanza Albert Kassa amesema alifanikiwa kukopa Sh 500 000 na kuweza kufanyia biashara zake na kuirejesha benki.
‘’Kumekuwa na changamoto kubwa sana ya wafanyabiashara wenzangu kuchukua pesa na kushindwa kuitumia katika inavyotakiwa’’ alisema Kassa.
Amesema mikopo ya NMB imekuwa ikiwasaidia sana wafanyabiashara katika biashara zao za kila siku. Alisema mpaka sasa mkoa wa Mwanza kuna wanachama 400 wa klabu ya biashara ya benki ya NMB.