Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara 15 wa Tanzania kushiriki maonyesho Uturuki

Uturuki Pic Wafanyabiashara 15 wa Tanzania kushiriki maonyesho Uturuki

Mon, 17 Oct 2022 Chanzo: Mwananchi

Wafanyabiashara 15 ambao ni wanachama wa klabu za biashara za benki ya NMB (NMB Business Club), wameondoka nchini kwenda Uturuki kushiriki Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (Trade Fairs 2022.

Maonyesho hayo ya siku tisa yanafanyika jinini Istanbul, Uturuki huku lengo la benki hiyo ni kuhakikisha wanachama hao wanapata ujuzi mpya katika kuendesha biashara.

Hafla ya kuwaaga wanachama hao imefanyika Makao Makuu ya NMB, ambako Afisa Mkuu wa Mikopo wa benki hiyo, Daniel Mbotto, amesema hii ni mara ya pili kwa taasisi yake kuratibu ziara za aina hiyo, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2019, ambako wafanyabiasahara 10 walitembelea na kushiriki Maonesho ya 125 ya Canton Fair 2019, jijini Guangzhou, China, kabla ya janga la corona kukwamisha safari hizo miaka miwili ya 2020 na 2021.

“Miongoni mwa maeneo watakayotembelea ni pamoja na viwanda vinavyozalisha bidhaa zenye soko kubwa nchini, ambazo wana uhusiano nazo, huko watajionea uzalishaji wa bidhaa zikiwemo vifaa tiba, ujenzi, nguo, vipodozi na kadhalika.

“Tunaamini ziara hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara hawa na taifa kwa ujumla wake, kwa kuwa kukua kwao kibiashara ni kuongezeka kwa ajira na manufaa kwa Watanzania wote,” amesema Mbotto

Hata hivyo, amesema kuwa wanachama hao wamepata fursa hiyo baada ya kukidhi vigezo ikiwemo kuangalia historia nzuri ya ukopaji na urejeshaji mikopo, kupitisha biashara zao kwa asilimia 95 katika benki ya NMB, kusaidia kwao kuunganisha wafanyabiashara kujiunga NMB na uwezo wa kuchangia asilimia kidogo za safari.

“Niwakumbushe zaidi wafanyabiashara, kuna fursa nyingi ndani ya benki yetu na msisite kutuchagua katika kufanya biashara kwa tija huku tukizingatia ubora zaidi kwa wateja wetu,” ameongeza.

Mwakilishi wa wafanyabiashara hao walio katika msafara huo, Paulo Lema, amesema wamekuwa wanufaika wakubwa wa huduma za benki hiyo kwa kuwa inawaongezea kuvu kubwa kiuchumi.

“Kadri NMB mnavyosapoti biashara zetu kwa kutupa mikopo, elimu ya fedha na fursa kama hizi, ndivyo mnavyoharakisha maendeleo na ustawi wetu kibiashara, tunawahakikishia Watanzania kwamba tutarejea tukiwa bora zaidi kutokana na matunda ya ziara hii,” amesema.

Naye Award Mpandila, ambaye ni mwenyekiti wa NMB Business Club mkoa wa Dar es Salaam, amekiri ziara hizo kuwa na manufaa makubwa na kuwajenga wafanyabiashara nchini.

Chanzo: Mwananchi