Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanya biashara waomba maeneo kujenga viwanda

Maeneoo Pic Wafanya biashara waomba maeneo kujenga viwanda

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (TWT) wameiomba Serikali kuanzisha maeneo maalumu na kujenga majengo ya viwanda ili kuwavutia wawekezaji wengi wa ndani kuanzisha viwanda.

Wamesema wamekuwa wakipitia changamoto kuanzisha viwanda kutokana na gharama kuwa juu akisema, endapo Serikali itaanzisha majengo na kuwapangishia wafanyabiashara sekta ya viwanda ingevutia wawekezaji wengi.

Hayo yameelezwa leo Desemba 5, 2022 na Mjumbe wa bodi ya TWT, Elias Maruma katika mkutano andaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) uliowakutanisha wadau wa viwanda na Serikali kwa lengo la kujadili namna ya kutatatua changamoto zao.

Maruma amesema gharama za kununua eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda au kujenga kiwanda chenyewe ni gharama kubwa ambayo wakati mwingine mwekezaji hukata tamaa kabla ya kuanza uwekezaji.

"Majengo ya kuzalisha bidhaa za viwanda ni gharama, unaweza kuwa na Sh100 milioni zikaishia kwenye ujenzi, Serikali ni muhimu itenge eneo la kujenga majengo ya viwanda ambavyo wawekezaji watapangishwa na hii itawavutia wawekezaji wengi," amesema.

Mbali na hayo, Maruma ameiomba Serikali kupunguza utitiri wa kodi kwa wamiliki wa viwanda.

Amesema ili Tanzania isonge mbele ni lazima kuwepo kwa jicho la pekee kwenye kodi ambazo zikichambuliwa pekee zinaweza kufika 20.

"Mara VAT, leseni ya Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS), Kodi ya huduma ya fire, Kodi ya Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), kodi ya uzoaji taka, kodi ya Halmashauri, kodi ya bandari na nyinginezo nyingi lazima kodi hizi zipunguzwe," amesema.

Hoja hiyo imepokelewa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ali Gugu aliyekiri kuwepo kwa changamoto hizo akisema Serikali inaifanyia kazi.

Akizungumzia utiriri huo wa kodi pamoja na wafanyabiashara katika Zanzibar na Tanzania bara kutozwa kodi mara mbili, Ofisa Elimu kwa mlipakodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Adela Kahela amesema kodi zote zipo kisheria.

"Kazi ya TRA ni kusimamia sheria kama kuna changamoto tunapokea ili kufanyike mabadiliko ya sheria kwa mwaka ujao wa fedha,suala la kodi mara mbili iko hivi,

Kwa Tanzania anapaswa kulipa kodi ya asilimia 18 lakini kwa Zanzibar anapaswa kulipa kodi ya asilimia 15 kwahiyo ukikatwa kule asilimia 15 ukija huku bara utalipa asilimia tatu iliyobaki," ameeleza. Mwananchi. Fikiri Tofa

Chanzo: Mwanaspoti