Ushirikishwaji wa kutoa maoni na mapendekezo kwenye sekta ya dijitali umetajwa kuwa changamoto inayowakabili wadau wa sekta hiyo nchini.
Wadau wa sekta hiyo wamesema mbali ya kushirikishwa, pia wamependekeza maoni wanayoyatoa katika majukwaa mbalimbali wanataka yatekelezwe na watunga sera, lengo likiwa ni kuboresha miongozo, sheria, mfumo pamoja na miundombinu ya teknolojia.
Wakizungumza Februari 15,2024 kwenye jukwaa la mawazo ya kidijitali, lililoandaliwa na taasisi ya Jamii Forums lililohusisha muunganiko wa taasisi 24 za kutetea haki za kidijitali, wamesema lengo lao kubwa ni kuboresha gurudumu la teknolojia nchini.
Ziada Seukindo, Meneja wa Programu wa Jamii Forums amesema kwa sasa Serikali inafanya jitihada ya miundombinu akitolea mfano ujenzi wa minara, lakini amehoji watu wanatumiaje.
Amesema lazima kama nchi ijue nini cha kufanya, ili watu wanufaike na matumizi ya intaneti na majukwaa ya kidijitali katika kuboresha maisha yao.
Seukindo amesema ili kufikia yote hayo, jambo kubwa wanalotaka ni ushirikishwaji wenye tija wa wadau wa sekta hiyo.
“Tunataka Serikali itushirikishe kwenye mchakato kuanzia hatua za mwanzo ichukue maoni yetu na yafanyiwe kazi kwa kuwa wote tunasukuma gurudumu moja,” amesema.
Pia, Ofisa Programu wa Jamii Forums, Francis Nyonzo amesema jambo la kufanya ni kutoa elimu ya kidijitali, ili watu waelewe kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja hadi Taifa kwa ujumla.
Nyonzo, amesema bado kuna tofauti ya uelewa na utumiaji wa dijitali miongoni mwa watu nchini, hivyo suala lililopo ni kuifanya dijitali iende mbele kwa kuwekeza ili watu wasione ni adui, bali ni fursa.
"Tukishaona kuwa dijitali sio adui hivyo kutakuwa na sera zitakazoakisi ukuaji wa dijitali," amesema.
Hata hivyo, ili kuingia uchumi wa kidijitali kunapaswa kujua changamoto zilizopo katika sekta hiyo ili kutatuliwa kama anavyosema Dk Patricia Boshe, Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Passau kilichopo Ujerumani.
Dk Boshe amesema utayari ndilo jambo la kwanza kwa wadau na watunga sera, ili kutengeneza imani kwenye matumizi ya mtandao kwa ujumla.
Wakati wadau hao wakiyasema hayo, Mkurugenzi wa Tehama Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Mashaka amesema Serikali inazingatia ushirikishwaji, hivyo inakuja na sera mpya ya Tehama ya mwaka 2024.
Ameongeza katika sera hiyo iliyo karibu kuidhinishwa wamezingatia ulinzi wa taarifa binafsi, teknolojia mpya zinazoibuka na usalama kwa wanawake na watoto wanapoingia mitandaoni.
Amesema hivyo mwelekeo wa sasa ni kushirikiana na sekta binafsi kutengeneza uelewa kwa jamii katika kipindi hiki ambacho uchumi wa kidijitali unashika kasi.
"Tumetayarisha mwongozo wa matumizi bora ya Tehama Tanzania ambao unaonyesha mambo mazuri na mabaya ya kuyaepuka. Tutautoa hivi karibuni ili wananchi wawe na uelewa juu ya matumizi ya teknolojia," ameeleza.