Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wataja mambo 10 utekelezaji mwongozo wa uwekezaji nchini

11118 Wadau+pic TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jumuiya ya wafanyabiashara nchini imependekeza mambo 10 yatakayosaidia utekelezaji wa mpango wa uboreshaji mazingira ya uwekezaji nchini.

Mwaka jana, Serikali iliandaa mpango huo kwa kukusanya maoni ya wafanyabiashara kutoka kwenye jumuiya tofauti ili kuboresha mazingira ya uanzishaji, usimamizi na uendelezaji wa biashara nchini.

Serikali ilifanya hivyo kutokana na malalamiko yaliyokuwapo pamoja na ripoti ya urahisi wa ufanyaji biashara inayotolewa na Benki ya Dunia kila mwaka kuonyesha Tanzania inashuka kwenye msimamo huo.

Wadau hao wamependekeza kuwapo kwa nidhamu ya utekelezaji kwa watakaopewa dhamana ya kufanya hivyo, kuandaa mpango kazi na kuweka vipaumbele katika mabadiliko yatakayofanywa.

Kingine ni kufanya tathmini ya mabadiliko ya sera, uendelevu wa utekelezaji wa maazimio yatakayopitishwa na kuwapo kwa mfumo wa kisheria kusimamia mabadiliko yatakayofanywa.

Vilevile, wadau hao wamependekeza kuwapo kwa kikosi kazi kitakachojumuisha sekta binafsi na ya umma, kanuni zinazotekelezeka na kuzingatiwa kwa maoni ya mwongozo huo kwenye bajeti ya Serikali.

Kutokana na maoni ya wadau yaliyomo kwenye mwongozo huo ambao uliwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri mwishoni mwa Mei, Serikali inatarajia kuondoa matakwa yanayojirudia baina ya mamlaka za usimamizi na sera zinazokinzana.

Akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wadau kutoka taasisi tofauti, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema ili kupata mafanikio ya mwongozo huo, utekelezaji jumuishi unahitajika.

Alisema taasisi hiyo iko tayari kutoa watu watakaofanya kazi pamoja na wizara na mamlaka nyingine za Serikali kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji vinaimarishwa.

“Ni jukumu letu kuikumbusha Serikali kuandaa mpango mkakati haraka iwezekanavyo ili kuutekeleza mwongozo huo,” alisema Simbeye.

Katika kuonyesha utayari, Simbeye alisema wameandaa wataalamu wa sekta tofauti wanaoweza kushirikiana na mamlaka za umma kuweka mazingira rafiki ya mabadiliko yanayotarajiwa.

Licha ya kukusanya maoni ya wadau wa sekta binafsi na jumuiya za kimataifa kisha kuridhiwa na Baraza la Mawaziri, mwongozo huo haujaidhinishwa na haujatengewa fungu lolote kwenye bajeti ya mwaka huu ili kuanza utekelezaji wake.

Ofisa mtendaji mkuu wa Jukwaa la Watendaji Wakuu (CEOrt), Santina Benson alisema ili matokeo ya mwongozo huo yaonekane, Serikali haina budi kuweka mpango mkakati wa utekelezaji.

Mpango mkakati huo, alisema unatakiwa uainishe usimamizi wa utekelezaji wa mwongozo na uwajibikaji utakaoihusisha pia sekta binafsi.

“Changamoto nyingi za ufanyaji biashara ni mtambuka. Tunatakiwa kuwa na picha pana ya vipaumbele katika utekelezaji wa mwongozo huu utakaozingatia sekta zote za uchumi,” alisema Santina.

Wadau hao walisema uangalifu mkubwa unahitajika katika ubadilishaji wa sera na kanuni ambazo zinaonekana kukwaza urahisi wa biashara nchini, ili kuondoka kwenye mtazamo wa kuongeza mapato ya Serikali badala yake zisaidie kushamiri kwa uwekezaji.

Katibu mtendaji wa Chama cha Viwanda vya Nguo (Tegamat), Adam Zuku alishauri juu ya kutungwa kwa sheria itakayoongoza utekelezaji wa mwongozo huo ili kupata matokeo chanya na endelevu. Pia, alishauri iwekwe bayana wizara itakayosimamia utekelezaji ili kuondoa mwingiliano wa majukumu kama uliopo sasa hivi baina ya Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji na Ofisi ya Waziri Mkuu zinazoonekana kuuchangamkia mwongozo huo.

“Ukitekelezwa kwa ufanisi, mwongozo huu utachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na kimataifa,” alisema Zuku.

Chanzo: mwananchi.co.tz