Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wamzungumzia bosi mpya CRDB

18449 Pic+crdb TanzaniaWeb

Sat, 22 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya bodi ya CRDB kumtangaza Abdulmajid Nsekela kumrithi Dk Charles Kimei ukurugenzi wa benki hiyo, wadau wamesema mtoto amerudi nyumbani akiwa na maarifa ya ziada.

Nsekela anajiunga tena na Benki ya CRDB akitokea NMB alikokuwa mkuu wa kitengo cha wateja wadogo tangu 2015. Lakini, kabla ya kujiunga na NMB, mtaalamu huyo wa sekta ya fedha alitoka CRDB alikodumu kwa zaidi ya miaka 10. Mchumi na mtafiti mwandamizi nchini, Profesa Samwel Wangwe alisema mabadiliko ya uongozi wa juu yaliyofanywa na CRDB yatasaidia kuongeza ubunifu wa taasisi hiyo kubwa ya fedha.

“Aliondoka wakati CRDB inafanya vizuri. Ameenda NMB yenye ubunifu mkubwa. uzoefu alioupata huko utamsaidia na tayari anaijua CRDB. Amerudi nyumbani akiwa na uzoefu mwingine utakaosaidia kuchochea maendeleo ya benki hiyo,” alisema Profesa Wangwe.

Uzoefu alionao Nsekela unawatoa wasiwasi wadau wa huduma za fedha na kuamini ataisaidia CRDB kufanya vyema zaidi.

Kamishna wa bima nchini, Dk Baghayo Saqware alisema hana wasiwasi na utendaji wa mkurugenzi huyo mpya kwa sababu anamfahamu tangu wakiwa wanafunzi wa stashahada ya juu katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). “Nampongeza Majid. Ni mtaalamu wa wasuala ya fedha. Naamini atakuwa na mchango mkubwa kwenye sekta hiyo akishirikiana na menejimenti ya CRDB. Sisi (Mamlaka ya Udhibiti wa Bima-Tira) tutampa ushrikiano wa kutosha,” alisema.

Dk Saqware alisema walikuwa pamoja wakati wanasoma Chuo cha Usimamiazi wa Fedha (IFM) kati ya mwaka 1996 na 1999, Nsekela akisoma uhasibu naye uhifadhi wa jamii.

Nsekela ataanza majukumu yake katika Benki ya CRDB kuanzia June mwakani. Kwa mujibu wa utaratibu wa benki hiyo kuanzia Januari Mosi mpaka Mei 31, 2019 atakuwa anakabidhiwa ofisi na Dk Kimei anayemaliza muda wake.

Anarudi kujiunga tena CRDB baada ya kuondoka zaidi ya miaka 10 iliyopita alipoihama benki hiyo na kujiunga na Benki ya NMB mwaka 2008.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa CRDB, Ally Laay inasema mteule huyo ana ufahamu wa kutosha kusimamia na kuongoza taasisi za fedha na amekuwa mbunifu wa bidhaa na huduma tofauti kwa kipindi alichohudumu kwenye sekta hiyo.

“Nsekela ana uzoefu zaidi ya miaka 20 kwenye sekta ya benki; biashara na udhibiti,” inasomeka sehemu ya taarifa ya mwenyekiti huyo.

Mkurugenzi mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker familia inayoachwa nyuma na Nsekela ina furaha kutoa kiongozi mkubwa anayejua namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo sokoni.

“Kinachotufurahisha zaidi nikuona uzoefu alioupata NMB umemuwezesha kuwa mkurugenzi mtendaji wa CRDB. Tunamtakia kila la kheri. Soko lina ushindani, kinachohitajika ni kufanyakazi pamoja kusaidi akukuza uchumi wa nchi na kuondoa changamoto zinazoikabili seka ya fedha nchini,” alisema Ineke.

Mabadiliko hayo ya uongozi wa juu wa benki hiyo kubwa zaidi nchini yanafanyika kumruhusu Dk Kimei kupumzika baada ya kuingoza kwa takriban miaka 21.

Dk Kimei aliyeiongoza CRDB kwa zaidi ya miaka 20 alitangaza dhamira yake ya kustaafu Desemba mwaka jana na Machi mwaka huu bodi ikatangaza kuanza kwa mchakato wa kumtafuta mrithi wake.

Wakati anatangaza dhamira hiyo, Dk Kimei alisema anajipanga kwenda kusimamia mambo yake binafsi lakini Rais John Magufuli akamuahidi uteuzi pindi atakapoondoka kwenye majukumu ya benki hiyo.

Rais alitoa ahadi hiyo mapema Machi alipokuwa anazindua tawi jipya la benki hiyo. “Nimesikia unatarajia kustaafu CRDB, Serikali bado inakuhitaji,” alisema Dk Magufuli.

Chanzo: mwananchi.co.tz