Siku moja baada ya Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) kukabidhi bandari hiyo kwa kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) ya Ufaransa kwa ajili ya kuiendesha, wadau wa bandari hiyo, wakiwemo vibarua na wachukuzi wameanza kuonja joto la mabadiliko ya ushuru.
Makabidhiano ya bandari yalifanyika juzi katika ofisi za ZPC, ambapo uendeshaji wa bandari hiyo utakuwa chini ya mwekezaji huyo kwa miaka mitano ili kuleta ufanisi na kuongeza mapato. Katika mkataba huo, mwekezaji atachukua asilimia 70 na Serikali asilimia 30.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wadau wa usafirishaji wa mizigo upande wa majahazi, walisema tayari ushuru umeongezeka mara mbili na ilivyokuwa awali.
Hata hivyo, Ofisa uhusiano wa ZPC, Hassan Amr alisema hakuna ushuru ulioongezeka, bali baada ya mwekezaji kukabidhiwa rasmi jana, ameanza kufuata utaratibu kwa mujibu wa mikataba ya bandari iliyokuwapo awali.
“Tunaona ushuru unapanda ghafla bila hata kuelezwa wala kushirikishwa wakati hapa kuna mizigo inayotakiwa kushushwa, lakini imeshindikana kwa sababu ya ongezeko hilo,” alisema Makame Khamis, wakala wa usafirishaji upade wa majahazi bandarini hapo.
Makame alisema ushuru wa kuingiza gari aina ya Toyota Canter ndani ya bandari kuchukua mizigo, ilikuwa Sh56,000, lakini jana wameambiwa walipe Sh100,000, akidai ni jambo la kutisha.
Alisema ipo haja kwa Serikali kuliangalia hilo kwa kina kwa sababu mawakala wanategemea eneo hilo kupata kipato.
Wakala mwingine, Omar Makame alisema wamepokea ugeni (mwekezaji) kwa uchungu mkubwa, maana huenda uchumi wao ukayumba.
“Bandari inabeba watu wengi, uchumi wetu upo hapa, familia zinatutegemea, lakini kupaa kwa ushuru ghafla kunatuweka katika mazingira magumu,” alisema.
Hata hivyo, alisema si kwamba hawaungi mkono uwekezaji huo, lakini kuna haja ya kuangalia upande mwingine wa wazawa wasije kupoteza vipato vya kuendesha uchumi wao.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Ushirika wa wachukuzi bandarini hapo (Dhow), Yahaya Andrew Pima alisema wachukuzi wanapata kipato kadiri wanavyobeba mizigo, lakini wasipofanya hivyo, hawapati kitu, hivyo jambo hilo huenda likawaathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu kuna hatari ya wenye magari kupunguza biashara ya kubeba mizigo bandarini hapo.
Lakini Ofisa Uhusiano wa ZPC, Hassan alisema hakuna ushuru ulioongezeka bali hizo ndizo bei halisi ila watu walizoea kupita njia za mkato.
Mchukuzi, Said Haji alisema uchumi wao unategemea bandari hivyo iwapo hali hiyo ikiendelea wataathirika.