Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau waibana Serikali kutafuta suluhu ya mafuta

Mafuta Pic Data (2) Wadau waibana Serikali kutafuta suluhu ya mafuta

Thu, 12 Oct 2023 Chanzo: mwanachidigital

Wachambuzi wa masuala ya kijamii wameibana Serikali kuhakikisha inatafuta mbadala wa changamoto bya mafuta badala ya kujificha katika kivuli cha changamoto za soko la dunia.

Wamesema sababu zinazoendelea kutolewa na Serikali hazina mashiko kwa wananchi huku wakihoji umuhimu wa kuwepo Kampuni ya TanOil inayojihusisha na biashara ya mafuta pamoja na mpango wa kurejesha uhai wa Kampuni ya kuhifadhi mafuta (TIPER).

Wametoa kauli hiyo leo Oktoba 11, 2023 wakati wa mjadala wa Mwananchi Space, ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Mjadala huo unafanyika ikiwa ni siku tisa zimepita baada ya Ewura kutangaza mabadiliko ya bei kikomo za mafuta ya petrol, dizeli zilizopanda kati ya Sh50 hadi Sh70 kwa kila lita katika mikoa yote nchini.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), inasema sababu za kupanda bei hizo ni kutokana na kupanda gharama za mafuta kwa hadi kufikia asilimia 4.21 na gharama za uagizaji wa mafuta hadi kufikia asilimia 17 kwa petroli, asilimia 62 kwa dizeli na asilimia nne kwa mafuta ya taa.

Pia, kuna uamuzi wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani (OPEC+) kupunguza uzalishaji na vikwazo vya kiuchumi ambavyo nchi ya Urusi imewekewa na mataifa ya magharibi.

Jumuiya ya wazalishaji wakubwa wa mafuta (OPEC) inamiliki takribani asilimia 80 ya soko la mafuta dunia. Jumuiya hiyo inahusisha mataifa 13; Kuwait, Libya, Iran, Iraq, Nigeria, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Venezuela, Angola, Gabon, Algeria, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Equatorial Guinea.

Baadhi wamehoji kwa nini Serikali isirejeshe ruzuku na kuondoa tozo zilizopo kwenye mafuta, hoja iliyojibiwa na msemaji wa Ewura , Titus Kaguo kwamba uamuzi huo ni mgumu kutokana na gharama zinazotumika kuagiza, kuratibu na kusambaza kwa wananchi.

Wengine wametaka kufahamu umuhimu wa kuwepo Ewura katikati ya changamoto ya mafuta iliyokosa majibu lakini Kaguo amesema tangu kuwepo kwa mamlaka hiyo imewezesha kupunguza angalau asilimia 30 ya bei ambayo ilitakuwa kuwepo juu ya kila lita.

“Bei ni sehemu ndogo ya majukumu ya Ewura, mamlaka hii inakuwa katikati kuhakikisha bei inakuwa ile inayotakiwa kuwa, “amesema Kaguo akisisitiza bila uwepo wao hali ingekuwa mbaya ya bei holela.

Kbala ya kujibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa, Kaguo ameanza kwa kueleza sababu za kupanda bei za mafuta katika soko kupitia sababu za wazalishaji wa mafuta OPEC, changamoto za uhaba wa dola pamoja na vita ya Urusi na Ukraine.

Akichangia hoja hiyo, mchambuzi mwingine wa masuala ya kijamii, Deogratius Andrew ameshauri maeneo matatu ikiwamo kupunguza urasimu katika uagizaji mafuta badala ya kuagiza kipitia madalali “Tuagize moja kwa moja kwenye nchi zinazozalisha mafuta.”

“Kingine ni muhimu kurejesha uhai wa Kampuni ya kuhifadhi mafuta (TIPER) ili tuagize mafuta gafi sio yaliyosafishwa, tusafishe hapa hapa itapunguza gharama,” amesema Andrew.

Tayari Wizara ya Nishati Tanzani imesema imepata eneo Kigamboni kwa ajili ya uwekezaji wa kituo kikubwa cha kupokea na kuhifadhi mafuta kitakachokuwa na uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 350,000 katika awamu ya kwanza ikiwa ni hatua ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Ameshauri hatua za muda mrefu ni pamoja na kuwa na nishati mbadala ikiwamo mfumo wa matumizi ya gesi mgandamizo kwenye magari (CNG), kama ilivyopendekezwa na wadau wengine.

Mchambuzi wa masuala ya biashara, Kairo Jamhuri amesema mfumuko wa bei kila mara imeshakuwa ni mazoea, nchi hii ina mifumo mingi ya upatikanaji wa nishati kama gesi asilia, kwanini sera za nchi hazionyeshi jitihada kuyafikia hayo maeneo.

“Kadhia mafuta ni kubwa sana, kufungia watu au vituo haitoshi kupunguza bei ya mafuta, mazingira ya biashara yategemea moja kwa moja upatikanaji wa nishati hii, kuna namna ambavyo wananchi wanatakiwa kushirikishwa kutoa mawazo yao ili kupunguza kadhia ya mafuta,” amesema.

Chanzo: mwanachidigital