Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wafundishwa mbinu upatikanaji wa fedha na usimamizi kuepuka hatari ya upotevu

70045 Pic+kongamano

Mon, 5 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kukuza uchumi wa wananchi sambamba na kusaidia kufanikisha ujenzi wa miradi mikubwa inayoendelea kujengwa nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Hazina na Masoko wa NBC, Peter Nalitolela amesema hayo leo wakati akizungumza katika  kongamano la wadau  juu ya upatikaji wa fedha  na usimamizi wa hatari zinazoweza kujitokeza katika miamala ya kifedha lililoandaliwa kwa wadau mkoani Dodoma.

Amesema benki hiyo imejizatiti kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi zake kuhakikisha nchi inafaidika na kiasi cha pesa inachotumia katika  miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kufanyika.

Amesema kongamano hilo linalohudhuriwa na wadau kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tanesco, TPDC na Wizara ya Fedha na Mipango, lina lengo la kuangalia vyanzo mbalimbali vya fedha vinavyopatikana katika miradi mbalimbali mikubwa inayofanywa nchini.

 Pia, linalenga  kuangalia usimamizi wa hatari katika miamala ya kifedha inayoweza kutokea katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Baadhi ya miradi mikubwa inayofanywa nchini ni pamoja na Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa Umeme wa Mto Rufiji wa Stiegler’s  Gorge na  ujenzi wa barabara na madaraja.

Pia Soma

“Kama mjuavyo baadhi ya miradi hufanywa kwa mikopo kutoka pande tofauti, hivyo tulitaka kuonyesha uwezo wetu kama NBC katika kusaidia upatikanaji wa fedha na pia linapokuja suala la usimamizi wa hatari za kifedha katika miamala hiyo,” alisema Nalitolela na kuongeza;

“Kikubwa ni kwa NBC kuangalia uwezo wetu kwa njia tofauti tofauti ikiwemo katika kukopesha, lakini pia kuona serikali haipati hasara kutokana na masuala ya riba, fedha za kigeni na kushuka kwa thamani ya shilingi, kwa uwezo wetu tunaweza kushirikiana zaidi na zaidi.”

Mkurugenzi huyo amesema kama inavyofahamika kuwa NBC inamilikiwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania, Benki ya Absa ya Afrika Kusini pamoja na Benki ya Dunia, hii huiweka NBC katika nafasi nzuri ya kusaidia juhudi za serikali.

Katika kongamano hilo pia NBC imeleta wataalam kutoka benki mama ya Absa ili kuweza kuonyesha uzoefu wao walioupata kupitia miamala waliyofanya na serikali za nchi mbalimbali barani Afrika.  

Chanzo: mwananchi.co.tz