Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wa korosho wavutiwa huduma ya NBC Shambani

Efeb46782fd6d070ac9d362a9e69e586 Wadau wa korosho wavutiwa huduma ya NBC Shambani

Tue, 18 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WADAU wa zao la korosho nchini, wameonesha kuvutiwa na huduma mpya ya ‘NBC Shambani’.

Wamebainisha kuwa huduma hiyo maalumu kwa ajili ya wakulima, itaondoa changamoto za muda mrefu ikiwemo kutopata mikopo kwa wakati sahihi.

Wadau hao ambao ni wakulima, wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo na wasafirishaji wa zao hilo, walibainisha hayo walipotembelea banda la huduma za benki hiyo kwenye mkutano mkuu wa wadau wa korosho, uliofanyika mkoani Lindi.

Walisema miongoni mwa changamoto zinazowakabili sasa ni kutopata mikopo kwa wakati, hivyo wanaamini ujio wa huduma hiyo mpya utaondoa changamoto hiyo.

“Licha ya uwepo wa huduma nyingi za kibenki kwa ajili ya wakulima, bado tumeendelea kukabiliwa na changamoto kadhaa za huduma za kifedha ikiwemo ucheleweshwaji wa mikopo na tunapoipata inakuwa sio wakati sahihi na hivyo kusababisha wengi wetu kuitumia kwa matumizi yasiyokusudiwa,”alisema mkulima wa korosho wa wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Salum Muhila.

Akifafanua kuhusu huduma hiyo kwa wadau hao, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na wa Kati kutoka NBC, Raymond Urassa alisema inalenga wadau wote wanaojihusisha na mnyororo wa biashara ya mazao ya kilimo.

Alisema wadau hao ni wasambazaji wa pembejeo za kilimo, wakulima na wasafirishaji wa mazao ya kilimo na tayari imeanza kutumiwa kwa wingi na wakulima wa zao la ufuta.

“Kwa kuwa ‘NBC Shambani’imekuja mahususi kwa ajili ya wadau wa kilimo, tafsiri yake ni kwamba ufanisi wake upo kwenye kutatua changamoto hasa zinazowagusa wadau hao ikiwemo kupata mikopo kwa wakati sahihi ili mkulima autumie mkopo huo kufanya kile kinachotakiwa kufanywa kwa wakati huo,’’alisisitiza.

Alibainisha huduma hiyo inatoa fursa kwa wadau hao kuwa na akaunti ya vikundi vya wakulima, kama vile AMCOS na vikundi vingine na akaunti ya mkulima mmoja mmoja.

“Akaunti ya ‘NBC Shambani’kwa vikundi vya wakulima inawawezesha kuweka fedha bila ada ya uendeshaji wa akaunti, vikundi vikifaidika kwa faida nyingi ikiwemo kutokatwa gharama za uendeshaji wa akaunti kila mwezi, kupata taarifa za akaunti bure na kutokatwa makato ya kuhamisha fedha wakati wa kulipa wakulima wenye akaunti NBC,”alifafanua.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alibainisha kuwa katika kukabiliana na changamoto kadhaa zinazowakabili wakulima, ikiwemo kutotambulika rasmi kwenye taasisi za kifedha, tayari serikali imeanza kutoa vitambulisho maalumu vitakavyowatambulisha hususani wanapohitaji huduma za kifedha.

“Vitambulisho hivyo vya kisasa vitakuwa na ‘chip’maalumu itakayobeba taarifa zote muhimu kuhusu mkulima, hatua ambayo tunaamini itarahisishia taasisi za fedha mlolongo mrefu wa kukusanya taarifa za wadau hao na hivyo kuwapatia mikopo kwa wakati,’’alisema Hasunga, ambaye katika mkutano huo alikabidhi vitambulisho hivyo vya mfano kwa wakulima 15 wa awali.

“Zaidi pia kwa sasa serikali tunatathimini upya sera ya masoko ikiwemo suala zima la kilimo cha mkataba ili wakulima wetu waweze kujua bei za bidhaa zao mapema,’’alibainisha.

Chanzo: habarileo.co.tz