Wadau wa ufugaji nyuki nchini wametakiwa kutumia fursa ya mkutano wa Dunia wa Ufugaji Nyuki (APIMONDIA) utakaofanyika nchini 2027, kuvutia wawekezaji na kuongeza tija katika ufugaji na biashara nzima ya mazao ya nyuki na utalii.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki katika mkutano na vyombo vya habari uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam .
"Tumieni mkutano huu vizuri kwa kuongeza tija katika ufugaji na biashara nzima ya mazao ya nyuki, kuongeza wigo wa mashirikiano na taasisi mbalimbali duniani katika kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo pamoja na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za ufugaji nyuki hususani teknolojia na mbinu mbalimbali za kuboresha na kuendeleza sekta hii "- amesema Kairuki.
Ametoa wito kwa watanzania na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuwa kwa sasa uzalishaji wa asali ni tani takribani elfu 32 tu wakati kama taifa kuna uwezo wa laki 138.
APIMONDIA ni Shirikisho la Umoja wa Vyama vya Wafugaji nyuki Duniani lililoanzishwa mwaka 1895 nchini Italia. Tanzania ilijiunga katika shirikisho hilo mwaka 1984 ambapo Tanzania kwa mwaka huu iliibuka kuwa mshindi wa kinyanganyiro cha kuandaa Mkutano wa 50 mwaka 2027.