Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau mkonge kumpa tuzo JPM

22827 Pic+mkonge Wadau mkonge kumpa tuzo JPM

Sun, 12 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WADAU wa zao la mkonge, wanatarajia kumpa tuzo Rais John Magufuli kwa kuinua zao hilo nchini kabla ya kumaliza kipindi chake cha pili cha uongozi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Rehema Nchimbi, katika kikao cha wadau wa zao hilo kilichofanyika jijini hapa jana, aligusia nia ya kutolewa kwa tuzo hiyo.

Alisema kwa kipindi kifupi cha utawala wake, Rais Magufuli amefanya jitihada za kuinua zao hilo.

Mkuu huyo alisema kuwa zao hilo miaka ya nyuma ndiyo lilikuwa linaongoza kwa kuliongezea taifa mapato, hivyo watahakikisha wanatumia mbinu zilezile kulirudisha zao hilo kwenye ubora wake.

"Kipindi cha nyuma zao la mkonge lilikuwa linaongoza kwa kuliongezea mapato taifa kwa asilimia 65, hivyo mkakati uliopo sasa ni kulirudisha zao hilo na kushika nafasi ya kwanza katika uzalishaji nchini,” alisema.

Nchimbi alisema kuwa, katika utawala wa Rais Magufuli, mambo ambayo yalidhaniwa hayawezekani, yamewezekana.

"Unajua hapa Dodoma ndiyo madhabahu ya Rais Magufuli ambaye alimwomba Mungu yakafanyika mambo makubwa katika muda mfupi, sasa na sisi tutumie madhabahu hiyo hiyo kufufua za la mkonge,”alisema Nchimbi.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge, Saad Kambona, alisema kuwa wameweka mkakati ya kuinua zao hilo kwa kuwashawishi wakulima wadogo kulima zao hilo ili uzalishaji uongezeke kwa kasi.

“Unajua baadhi ya watu wanafikiri kilimo cha mkonge kinafanywa na wakulima wakubwa tu, siyo kweli, hata wakulima wadogo wadogo wakifanya kilimo hicho kwa wingi, uzalishaji utakuwa mkubwa na serikali itaongeza pato la taifa,” alisema Kambona.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa hivi sasa, wanazalisha tani 36,000 ambapo mkakati uliopo ni kuzalisha tani 120,000 hadi 150,000 kwa mwaka.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, alisema serikali ina mpango wa kuinua zao hilo nchini, ili kuhakikisha linafikia malengo waliojiwekea.

Alisema serikali haitakuwa tayari kuona waliopewa viwanda wanaviatamia badala ya kuviendeleza ili kuwasaidia wakulima wa mkonge nchini.

"Serikali haitakuwa tayari kuwavumilia wenye viwanda ambavyo hawavifanyii kazi, tayari nimemwagiza Msajili Hazina aanze kuwasaka wanaoatamia viwanda," alisema Mgumba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live