Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) limeanza kukusanya maoni ya wadau wa usafirishaji kwa njia ya maji kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kujadili na kutoa maoni kuhusu gharama ya usafirishaji, ikiwemo nauli ya boti ya mwendokasi ya Mv Rafiki 2 inayosafirisha abiria kati ya Mwanza na Bukoba.
Boti hiyo inayomilikiwa na kampuni binafsi ya Songoro Marines ya jijini Mwanza ina uwezo wa kubeba abiria 328 na inatumia muda wa saa nne kusafiri kati ya Mwanza na Bukoba.
Nauli ya awali wakati wa safari za majaribio ilikuwa kati ya Sh30,000 hadi Sh60,000 kwa watu wazima, huku watoto wakitozwa kati ya Sh17,500 na Sh30,000 kwa safari.
Kwa mujibu wa chati ya nauli, abiria wa daraja la kati wanalipa Sh35,000 kwa watu wazima, wakati watoto wanatozwa Sh17,500, huku wenye ulemavu wakilipa Sh30,000 kwa safari.
Katika daraja la juu, watu wazima wanatozwa Sh50,000, wenye ulemavu Sh40,000 na watoto Sh22,500, huku nauli ya daraja la kwanza ikiwa ni Sh60,000 kwa watu wazima, wenye ulemavu Sh50,000 na watoto ni Sh30,000.
VIDEO: Wadau kujadili nauli za mwendokasi Ziwa Victoria
Kutokana na maombi ya wananchi kwa Serikali kuangalia viwango hivyo vya nauli kuwezesha watu wengi kutumia usafiri huo, Tasac imeanza kupokea maoni ya wadau katika mikoa ya Mwanza na Kagera kabla ya kutoa bei elekezi ya nauli ambapo wananchi wameombwa kujitokeza kutoa maoni yao kuanzia Januari 5 hadi Januari 13.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau uliofanyika jana jijini Mwanza, Mkurugenzi Udhibiti Uchumi wa Tasac, Nahson Sigalla alisema maoni hayo yanapokelewa kwa maandishi (baruapepe) au kupitia mikutano ya wadau itakayofanyika katika mikoa ya Mwanza na Kagera.
Mdau wa usafirishaji kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki (Taec), Baraka Kajubu alishauri upangaji wa bei elekezi kuzingatia hali halisi ya kiuchumi ya wananchi, huku akipendekea nauli isitofautiane sana na ile inayotozwa kwenye meli za Serikali na mabasi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marines, Major Songoro alisema bei ya nauli inazotozwa wakati huu wa safari za majaribio imezingatia gharama za uendeshaji kuwezesha huduma hiyo siyo tu kuwa endelevu, bali pia ijiendeshe kwa faida.