Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadaiwa sugu TBA kusakwa kidigitali

Wadaiwa Tba Tba (600 X 336) Wadaiwa sugu TBA kusakwa kidigitali

Thu, 2 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameupongeza Wakala wa Majengo Nchini (TBA) kwa kuweka mfumo wa kisasa wa kidigitali kwenye kitasa janja (Smart Lock) unaoruhusu mpangaji kuingia ndani kwa kutumia kadi ambayo imeshalipiwa ambapo awali walikuwa wakitumia nguvu na muda mwingi kukusanya kodi kwa wadaiwa sugu.

Amezungumza hayo jijini Arusha, mara baada ya kukagua maendeleo ya jengo la kitega uchumi linalojengwa na Wakala huo ambapo Waziri Profesa Mbarawa amesema jengo hilo litapunguza changamoto za makazi kwa watumishi wanaofanya kazi katika ofisi za Serikali Mkoani humo.

“Mfumo huu ni mzuri sababu ambaye hajalipa hatakuwa na uwezo wa kuingia ndani kwake lakini utawapunguzia sana usumbufu hongereni sana”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Aidha, ameupongeza Wakala huo kwa kukamilisha jengo hilo la ghorofa 10 lenye uwezo wa kuchukua familia 22 kwa kutumia fedha zao za ndani.

Naye Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Arusha Eng. Juma Dadi amemweleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa mpaka sasa TBA imeshapokea maombi takribani 40 ya wapangaji katika nyumba hizo hali inayowapa motisha ya uhitaji zaidi wa nyumba katika mkoa huo.

Jengo la Kitega Uchumi la Makazi mkoani Arusha limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.5 na kwa sasa limefikia asilimia 98 na linatarajiwa kukumilika mapema mwezi Aprili mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live