Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadaiwa sugu TBA kuondolewa kwa lazima Desemba Mosi

TBA Sig.png Wadaiwa sugu TBA kuondolewa kwa lazima Desemba Mosi

Thu, 23 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kama wewe ni mpangaji katika nyumba zinazomilikiwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA), na hujalipa kodi ya pango kwa muda mrefu, kaa chonjo kwani kuanzia Desemba Mosi mwaka huu wakala huo utawang’oa wadaiwa wote kwenye nyumba hizo, huku wakifunguliwa kesi za madai.

Kwa mujibu wa TBA, hadi kufikia Oktoba 31, 2023, taasisi hiyo inadai zaidi ya Sh7.8 bilioni za kodi ya pango kutoka kwa wapangaji hao, huku kati ya hizo Sh3.5 bilioni ni madeni toka kwa taasisi mbalimbali za Serikali.

Wadaiwa hao wenye madeni makubwa, wameifanya TBA kushindwa kutekeleza mipango ya ukarabati wa nyumba zilizopo na kujenga mpya zitakazopangishwa au kuuzwa kwa watumishi wa umma wanaokabiliwa na changamoto ya makazi.

Hatua ya kuwashughulikia wadaiwa hao imetangazwa leo Novemba 22, 2023 jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa TBA, Daud Kondoro.

Kandoro amesema kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wapangaji kwenye nyumba zinazomilikiwa na TBA kutolipa kodi kwa wakati na kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni, wengi wakiamini kwa kuwa ni nyumba za umma hawawezi kutolewa licha ya madeni hayo yasiyohimilika.

“TBA imeazimia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wapangaji wote tunaowadai. Tutawaondoa wadaiwa sugu kwa nguvu kwa kutumia dalali wa Mahakama ambao ndio wamepewa zabuni hiyo kwa niaba ya TBA,” amesema.

Tayari kampuni ya udalali wa Mahakama iitwayo WINS Auction Mart imeshakabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa ajili ya utekelezaji wa kuwaondoa, ambapo watafanya hivyo nchi nzima kuanzia Desemba mosi, 2023.

Pamoja na hatua ya kuwaondoa, TBA imesema itawaburuza mahakamani wadaiwa wote, huku ikisisitiza waliopewa namba za malipo zikiwemo taasisi za umma, kulipa madeni yao mara moja.

Pamoja na hayo, TBA inawataarifa wapangaji wake wote kwamba kuanzia Desemba mosi mwaka huu wataanza kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa Usimamizi wa Miliki za Serikali (GRMS) toleo la 2.

Mfumo huo mpya utakuwa unatoza riba ya asilimia 20 kwa mpangaji atakayekaa zaidi ya miezi mitatu bila kulipa kodi ya pango. Riba hiyo itaendelea kutozwa kila mwezi kwa kiwango cha asilimia 20 kupitia mfumo hadi deni lote litakapokamilika kulipwa.

“Utekelezaji huo ni kwa mujibu wa kifungu Na. 5.2 cha mkataba wetu wa upangishaji, tayari wakala umeshaanza kutumia vitasa janja kwenye majengo mapya ili kudhibiti malimbikizo ya kodi ya pango. Pia mpango huu wa kufunga vitasa janja utaendelea kutekelezwa kwenye nyumba zetu za zamani,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live