Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachumi wazungumzia ushauri wa IMF kuhusu tishio la hali ya benki

30804 Wachumi+pic TanzaniaWeb

Mon, 10 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baadhi ya wachumi wameitaka Serikali kunusuru sekta ya fedha  baada ya ripoti ya Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) kuonyesha hazina uwezo wa kukabiliana na mtikisiko wa kifedha duniani. Ijumaa IMF ilitoa ripoti ya tathmini ya hali ya kifedha nchini inayoonyesha kuwa karibu nusu ya benki 45 zilizopo nchini zinaweza kuanguka ikiwa dunia itakumbwa na mtikisiko wa kifedha. Shirika hilo liliishauri Tanzania kuboresha ubora wa mali, kushughulikia mikopo isiyolipwa na kuongeza kinga ya mtaji katika mfumo wa kibebenki. Tathmini ya IMF inayofanyika kila baada ya miaka mitano, ilionyesha mtisiko usio wa kawaida lakini wenye uwezekano wa kutokea ukichangiwa na mambo ya ndani na nje. “Mitikisiko hii husababisha  kupungua kwa kasi ya ukuaji uchumi, fedha kushuka thamani, mfumuko wa bei na kuathiri riba,” inasema tathmini hiyo. “Licha ya maendeleo yaliyopo, changamoto zilizopo si za kubeza. Ubora wa mali za benki na taasisi za fedha umepungua na tengo la hasara kuongezeka miaka ya hivi karibuni. Ukuaji wa mikopo umepungua pia.” Wakizungumza na Mwananchi jana, wachumi waliomba Serikali ichukue hatua. Mmoja wa wachumi hao, Humphrey Moshi alisema kuwepo kwa mikopo isiyolipika kutokana na benki hizo kutokuwa makini na wakopaji, hasa kwenye dhamana wanazoweka. “Kuyumba kwa benki kunasababishwa na kutofuata taratibu za mikopo. Mtu anakopa Sh400 milioni anaonyesha nyumba ya Sh20 milioni, wakati mwingine hata benki haiendi kuangalia,” alisema. “Au mtu anakopa Sh1 bilioni halafu anapotea. Benki ikifuatilia nyumba aliyoweka dhamana inapata Sh200 milioni.” Kuhusu madeni ya Serikali, Profesa Moshi alisema mengi yalikopwa na awamu zilizopita za urais na yalikopwa kwa hasara, lakini “madeni ya sasa yatalipika kwa sababu yanajengea miundombinu”. Profesa Moshi alisema licha ya sekta ya kilimo kuajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania, inatoa mchango mdogo kwa Pato la Taifa. Alisema mpango wa pili wa kilimo (ASDP 2) uliozinduliwa na Rais John Magufuli utabadilisha hali hiyo.  Mchumi mwingine alikosoa mipango ambayo alisema inawafanya wananchi wasiwe na fedha na hivyo kushindwa kukopa au kulipa mikopo yao. “Kilichoelezwa na ripoti hiyo ni sahihi kwa sababu athari za kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi zinajidhihirisha,” alisema mchumi mwandamizi nchini, Dk Abel Kinyondo. “Madeni mengi ya Serikali ambayo kimsingi siyo mabaya, yamechukuliwa kwa lengo kujenga miundombinu kama barabara na madaraja. Lakini cha kujiuliza kipaumbele ni nini? Je, ni kujenga tu madaraja bila kuangalia ubora wa elimu au afya? “Ukiuliza kuhusu elimu Serikali inasema inatoa elimu bure, je ubora wake ukoje? Kwa nini mzazi ampeleke mtoto wake kwenye shule zenye ada kubwa katika hali hii ya uchumi, aache elimu ya bure?” Alisema licha ya maendeleo ya miundombinu yanayofanyika kutokana na fedha za mikopo, kinachotakiwa ni kuoanisha na maendeleo ya watu kwa pamoja, akitoa mfano wa nchi ya Ethiopia kuwa imefeli kufanya hivyo ndio maana wananchi wanaikimbia licha ya Serikali kuwekeza katika miundombinu. Alisema licha ya Tanzania kutajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwasi, bado kipimo kinachotumiwa cha kupima pato ghafi hakitoi uhalisia wa hali ya uchumi.

Chanzo: mwananchi.co.tz