Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachumi watia neno uchumi kuimarika

9be54fc60ae6e5e3ba762d4d1c3f5f87 Wachumi watia neno uchumi kuimarika

Sat, 13 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATAALAMU wa masuala ya uchumi wameeleza kufurahishwa na mwenendo wa hali ya uchumi licha ya nchi kupitia changamoto za ugonjwa wa corona wakisisitiza kuwa hayo yamewezekana kutokana serikali kujikita kwenye utekelezaji wa mipango yake kwa vitendo.

Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili, wamesema kama ambavyo serikali imekuwa ikiweka wazi vipaumbele vyake hasa vile vinavyochangia ukuaji wa uchumi na matokeo yake kuonekana, wameunga mkono hatua ya kutenga fedha nyingi katika kufanikisha miradi ya kuchangia uchumi.

Akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa ukomo wa bajeti wa serikali kwa wabunge juzi jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango katika kuzungumzia mwenendo wa hali ya uchumi, alisema pamoja na changamoto zilizokumba dunia ikiwamo ugonjwa wa corona, uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mtaalamu katika Maendeleo ya Uchumi nchini ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa, Joseph Semboja alisema mafanikio hayo yaliyopatikana kwenye Serikali ya Awamu ya Tano yametokana na uwekwaji wa msisitizo kwenye utekelezaji kivitendo wa mipango iliyokusudiwa.

Profesa Semboja alisema nia yake ya kuamua kutekeleza kivitendo miradi mikubwa ya kiuchumi, serikali imejikuta ikifanikiwa kukuza uchumi kwa muda mfupi kutokana na kusimamia vipaumbele vyake.

Aliunga mkono taarifa ya Dk Mpango kwamba kukua kwa uchumi kumechagizwa na miundombinu ya barabara, madaraja, bandari, viwanda, mifugo na kilimo kama ambavyo tangu ilipoingia madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano ilinuia kuviimarisha.

“Kama ambavyo serikali imekuwa ikiweka wazi vipaumbele vyake hasa vile vinavyochangia ukuaji wa uchumi, sasa matokeo yake ndiyo haya yanayoonekana…Ninachoona hapa ni kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha vipaumbele hivi vinaongezwa na vinaendelea kusimamiwa,” alisema.

Profesa Semboja aliongeza, “Rais Magufuli amekuwa muumini wa viwanda na leo tumeweza kuzalisha vitu vikubwa ambavyo zamani ilikuwa ni lazima kuagiza nje na hivyo kusababisha fedha za nchi kupotea, ila kwa sasa tunauza nje bidhaa na tunapata hela na hiyo ni kutokana na uwekezaji wenye viwanda na mambo mbadala wa viwanda kama barabara, madaraja na itakayokuja kuwa Reli ya Mwendokasi (SGR)

” Profesa wa Uchumi, Honest Ngowi alisema ili kuwa na maendeleo endelevu kwenye mafanikio yaliyotajwa na Dk Mpango, upo ulazima wa Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye uendeshwaji wa miradi husika au kuwekeza kwenye viwanda.

Profesa Ngowi alisema kwenye viwanda kuna ushiriki wa wawekezaji kutoka nje na vivyo hivyo inapaswa na Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwenye viwanda vikubwa na vya kati kushiriki katika kuendesha uchumi.

Alitaja miradi kama vile wa SGR na kusema kwenye ngazi ya ujengwaji wake upo ushiriki mzuri wa Watanzania. Alisema inapaswa itakapokamilika wananchi waitumie kikamilifu kusafirisha mizigo.

“Mkakati ni mzuri na kama ambavyo utekelezwaji wa vipaumbele hivyo ulivyoelezwa na Dk Mpango kwa maana ya kuwa ilianza kuwekwa mikakati na kisha kuitengezea fedha kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vya mikakati hiyo, hivyo fedha nyingi sana zilitengwa na kutumika kwenye kufanikisha miradi ambayo sasa imekuja kuchangia kukua kwa uchumi.

Hii ni njia nzuri ya kuendeleza uchumi wa nchi,” alisema Profesa Ngowi. Akizungumzia taarifa ya waziri Mpango kuhusu sekta ya madini ilivyoimarishwa na kujikuta ikitoa gawio na Sh bilioni 100, Katibu Msaidizi wa Chama cha Madini Wanawake (Tawoma), Mecktilda Mchomvu alisema Serikali ya Awamu ya Tano imesaidia kuchagiza maendeleo ya sekta hiyo kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuanzishwa kwa Tume ya Madini kumesaidia kuwawezesha wanawake kushiriki kwa karibu zaidi kwenye biashara ya madini kwa kutokana na kujengwa kwa masoko 39 ya madini na vituo 41 vya kuuzia madini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz