Wakati kilio cha ongezeko la bei za petroli na dizeli kikizidi kupazwa, Serikali imeshauriwa ianze tena kutoa ruzuku ikiwa ni hatua ya muda mfupi, huku ikiweka mpango wa muda mrefu wa kutumia gesi.
Aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba Mei 10, mwaka 2022 alitoa tangazo la ruzuku ya Serikali ya Sh100 bilioni ili kupunguza makali ya bei ya mafuta nchini iliyoanza kutumika Juni mosi.
Kiasi hicho kilidumu kwa miezi mitatu mfululizo. Septemba 2022 Serikali ilipunguza kiwango cha ruzuku hadi Sh65 bilioni na Sh59.58 bilioni Oktoba.
Novemba na Desemba mwaka jana, Serikali iliendelea kuweka ruzuku kwenye bidhaa hiyo bila kutaja kiwango cha fedha. Kwa Desemba, bei ya rejareja ya petroli iliyoingia kupitia Bandari ya Dar es Salaam haikuwa na ruzuku. Baada ya hapo ruzuku iliondolewa kwenye bidhaa hiyo.
Ilivyo sasa, mwenendo wa bidhaa za mafuta katika soko la dunia unaonyesha uwezekano mdogo wa kupungua bei ndani ya miezi michache ijayo, huku bei zikizidi kupanda.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ongezeko la bei kwa mwezi huu limetokana na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia kwa hadi kufikia asilimia 4.21.
Wakati bei ya mafuta ikipanda, nchini kuna tatizo la upungufu wa umeme, hivyo kusababisha gharama za uzalishaji viwandani kuongezeka. Kutokana na hilo, mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi wa kawaida ndiye anayeumia zaidi.
Wasemavyo wachumi
Akizungumzia hali hiyo, Zitto Kabwe, kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo alisema, “kutatua hili kuna njia ya muda mfupi ambayo ni Serikali kuweka ruzuku, ila hili tukumbuke litapunguza Sh100 tu kwa kila lita, ijapokuwa sisi (ACT-Wazalendo) tulipendekeza kupunguza tozo ya Sh500 kwa lita.
“Hayo yote tunavyofanya lazima Watanzania wajue kuna huduma za kijamii zitaathirika, maana tunapunguza mapato. Njia mbadala na sahihi ni kugeukia nishati ya gesi, hapa tutaokoa fedha nyingi tunazotumia kununua mafuta kutoka nje ya nchi.”
Kwa upande wake, Profesa Aurelia Kamuzora, mchumi mwandamizi katika Chuo Kikuu Mzumbe, alishauri njia ya muda mrefu ni kuwekeza katika teknolojia ili kutumia nishati jadidifu, ikiwamo ya jua.
Alieleza wasiwasi endapo akiba ya nchi itatosheleza kupata fedha za kuweka ruzuku ili itumike kama njia ya kupunguza makali ya bei ya mafuta.
“Kuweka ruzuku katika bidhaa hii ni njia ya haraka ambayo inaweza kusaidia, lakini je, Serikali yetu imejipanga? Ina fedha za kutosha katika bajeti yake kwa sasa? Kwa nchi inayoendelea kama yetu nashauri tujikite kuwekeza katika teknolojia, ili nishati mbadala zitumike na tusitegemee mafuta pekee.
“Najua hii ni njia ya muda mrefu, lakini nchi za wenzetu kama China waliwekeza katika teknolojia na inawasaidia sasa katika nishati wanazotumia, ikiwamo ya umeme jua,” alisema.
Hata hivyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo alisema, “kwa sasa hakuna namna ya kuvuka hapa zaidi ya kuweka ruzuku na kuhakikisha umeme unapatikana. Hakuna nchi yenye bajeti inayojitosheleza, kitu cha msingi ni kuweka vipaumbele tu na kufahamu udharura wa jambo hili.”
Bei zinavyong’ata
Baadhi ya madereva wa usafiri wa umma maarufu kama daladala na wale wa bajaji na bodaboda waliozungumza na Mwananchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Iringa, Dodoma, Kilimanajro, Mbeya, Arusha na Mwanza, wanaeleza kuwa kupanda bei ya mafuta kumesababisha kipato chao kupungua na kutishia wengine kupoteza ajira.
Bajaji, bodaboda
Madereva wa bodaboda ambao wamekabidhiwa vyombo hivyo vya moto wakitakiwa kupeleka mapato kwa waajiri ya kati ya Sh35,000 na Sh70,000 kwa wiki wanasema baadhi wameshindwa kutimiza malengo kutokana na gharama ya mafuta kupanda.
Felix Shayo, dereva bodaboda mjini Mtwara anasema, “kazi yetu ni changamoto, unapata Sh25,000 kwa siku; unatumia Sh9,000 kwa ajili ya mafuta ambazo ni lita mbili na nusu. Sh10,000 unapeleka kwa bosi kila siku, unabakia na Sh6,000, ule na ufanye maendeleo mengine?” alihoji.
Katibu wa chama cha wasafirishaji kwa njia ya barabara mkoani Dodoma, Mussa Nsese ambaye ni dereva wa bajaji, alisema kwa sasa wanatumia mafuta ya Sh30,000 kwa siku kutoka kati ya Sh15,000 na Sh18,000 miezi kadhaa iliyopita.
Naye dereva wa daladala, inayoyafanya safari kati ya Bunju-Simu2000, Mathias Muhuna ameiomba Serikali kuingilia kati kwa kutoa ruzuku ya mafuta ili kuwapunguzia makali ya maisha.
Alisema awali kwa siku alikuwa anatumia mafuta ya kati ya Sh108,000 na Sh110,000, sasa anatumia Sh152,000 hadi Sh154,000. Mbali ya bei ya mafuta, anasema pia vipuri vimepanda bei.
Boniface Antony, anayefanya safari kati ya Gongo la Mboto-Simu2000, alisema kupanda kwa mafuta kumeathiri kipato chake kwa kuwa baada ya kumkabidhi mwajiri Sh100,000 kwa siku, awali alikuwa hakosi posho ya kati ya Sh80,000 na Sh100,000.
Alisema hivi sasa hupata kati ya Sh40,000 na Sh60,000, hivyo wakigawana na kondakta hupata kila mmoja kati ya Sh20,000 na Sh30,000. Pia kuna siku alisema hawaambulii chochote.
Wamiliki wa daladala
Thomas Awe, mmiliki wa daladala jijini Dar es Salaam alisema ongezeko la bei ya mafuta limemsababishia hasara, akilazimika kushusha hesabu ya mapato kutoka kwa madereva wake.
Locken Adolf, Katibu mkuu wa chama cha wasafirishaji wa abiria mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (Akiboa), alisema watakutana wiki ijayo kujadiliana na kuwasilisha serikalini maombi ya kupandisha nauli.