Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachumi wataja mwarobaini kupanda bei vifaa vya ujenzi

Vifaa Ujenzi Mwarobaini bei vifaa vya ujenzi watajwa

Thu, 10 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku moja baada ya Serikali kutangaza hatua kadhaa za kudhibiti kilio cha kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi, wachumi na wazalishaji wameshauri hatua ambazo zikichukuliwa zitapunguza kilio hicho na kufanya upatikanaji wa bidhaa hizo kuwa katika hali ya utulivu.

Hata hivyo, mchumi mbobevu Profesa Hamphrey Moshi alisema Serikali inachopaswa kufanya ni kuangalia uwezekano wa kupunguza tozo katika mambo yanayoathiri ukuaji wa sekta nyingi, akitolea mfano mafuta na pia kuimarisha uzalishaji wa dani ya bidhaa mbalimbali.

“Kunguza gharama za mafuta ili kurahisisha usafirishaji hususani wa ndani, tatizo la mafuta hata kama bei ikiongezeka kwa asilimia 10, unakuta wasafirishaji wanaongeza gharama za usafirishaji hata mara mbili,” alisema Profesa Moshi.

Alisema suala la kupanda kwa bei ya vitu mbalimbali ikiwemo vifaa vya ujenzi si la Tanzania pekee bali la duniani nzima na sababu inatajwa kuwa uwepo wa ugonjwa wa Uviko-19 ambao umeaathiri uzalishaji viwandani na usafirishaji.

“Gharama za usafirisaji zimeongezeka na hivi sasa si rahisi kusafirisha shehena moja kwa moja, unakuta kuna mizunguko mingi,” alisema Profesa Moshi akitolea mfano wa kifurushi chake alichotumiwa kutoka nchi za nje Sepetemba mwaka jana kikamfikia Februari mwaka huu.

Profesa Moshi alizungumzia umuhimu wa kuimarisha sera ya viwanda na kuhakikisha uzalishaji mkubwa wa bidhaa zinazohitaji hapa nchini zinazalishwa ndani ili hata dunia ikipata mtikisiko usambazaji ubaki katika utulivu lakini pia uwepo udhibiti wa ushindani wa sokoni.

Kwa upande mwingine, Dk Abel Kinyondo ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi, alisema kama kupanda kwa bei hakujatokana na nguvu ya soko, Tume ya Ushindani (FCC) inapaswa kufanya kazi yake vizuri ili kutokuwa na upandaji wa bei kiholela au kuvurugwa kwa soko.

“Mfano unaweza kujiuliza kwanini viwanda vya simenti vifunge kwa wakati mmoja kufanya matengenezo, hapo panaweza kusababisha shida, iwapo mtu atanunua bidhaa hiyo yote na kuiuza kwa bei ya juu,” alisema Dk Kinyondo.

Kuhusu suala la kuruhusu uingizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi kama mbadala wa kuongeza usambazaji, upatikanaji na kushusha bei ya bidhaa husika, Dk Kinyondo alisema “Hii inaweza kuwa njia bora ya kunusuru hali iliyopo lakini umakini unahitaji ili kutoua viwanda vya ndani,” alisema.

Hata hivyo , mhumi mwingine ambaye ni profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema suala la kulinda viwanda vya ndani ni wajibu wa Serikali sawa na ilivyo kulinda mlaji wa mwisho.

“Mlaji wa mwisho analindwa kwa kuruhusu uingizaji wa bidhaa husika lakini hatua hiyo iwe ya ya muda mfupi wakati ambapo viwanda vinajipanga kuzalisha zaidi.”

Ili kupunguza bei ya bidhaa sokoni, mtaalamu wa Sera za biashara wa Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI), Frank Dafa alisema Serikali iangalie uwezekano wa kuwapunguzia wazalishaji gharama za uendeshaji ili waweze kuwa shindani sokoni.

Dafa alisema mambo yanayolalamikiwa na wazalishaji ambayo yakifanyiwa kazi yanaweza kupunguza gharama za uendeshaji ni pamoja na miundombinu ya usafirishaji wa mali ghafi, upatikanaji wa nishati ya uhakika na gharama nafuu, ya umeme na gesi.

“Masuala ya miundombinu ya usafirishaji kama reli na bandari vikiimarishwa ili kurahisisha usafirishaji, gharama zitapungua kwa wazalishaji labda itabaki wauzaji na wasambazaji lakini kwa wazalishaji wa nondo wanalia na sheria inayowazuia kuingiza chuma chakavu ambacho kwao ni mali ghafi,” alisema Dafa.

Dafa alisema wazalishaji wa vifaa vya ujenzi, hasa wa nondo na saruji ,kwa muda mrefu hawajaongeza gharama za bidhaa zao licha ya kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, gharama huenda imepandishwa na soko kwa upande wa wauzaji na wasambazaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live