Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachumi na makali ya January

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baadhi ya wachumi wamesema mwezi wa kwanza (Januari) unaonekana kuwagusa kiakili na kihisia wazazi na walezi kutokana na kutokuwapo utamaduni wa kujiwekea akiba kwa Watanzania wengi.

Wachumi hao wamesema hayo wakati kukiwa na pilikapilika za wazazi wakipishana masokoni wakinunua vifaa vya shule kama madaftari, kalamu na sare za shule, huku suala kubwa likiwa ni ada.

Kama hiyo haitoshi, mwezi Januari pia wazazi wengi hukumbana na gharama nyingine kama kulipia bili za umeme, maji, ving’amuzi na kodi ya nyumba na kuwafanya kuwa na wakati mgumu

Kwa kuwa mwezi huo huja mara tu baada ya kumaliza msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na mwaka mpya ambazo watu hutumia fedha nyingi kwenye sikukuuu hizo hali huwa ngumu zaidi kutokana na kutozingatia Januari inakaribia na kwamba kutakuwa na mahitaji mengi.

Mwezi wa Januari wenye siku 31 unaonekana kuwachanganya zaidi wazazi na walezi ambao wanategemea kulipwa mishahara ya mwezi na wale wanaotegemea biashara ndogondogo na kilimo cha kujikimu.

Baadhi ya wataalamu wa uchumi wamezungumzia hofu hiyo wakitaka Watanzania wajenge utamaduni wa kujiwekea akiba na kupanga mahitaji ya mwaka ili kupunguza makali ya Januari.

Mtaalamu wa uchumi, Dk Donath Olomi amesema hali hiyo ni kwa sababu ya mahitaji mengi yanayowakumba watu kwa wakati mmoja.

Amesema ugumu wa Januari unakuja kwa sababu kabla yake Desemba watu wengi hutumia fedha nyingi kwenye mahitaji ya kifamilia.

“Kwa watu walio vizuri katika upangaji wanaweza kukabiliana na hofu hii inayokuja na mwezi huo. Ni muhimu kwa watu kufanya mipango ya mwaka mzima kulingana na vipato vyao,” amesema.

Profesa Samuel Wangwe ambaye ni mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anahusisha ugumu wa Januari na tabia ya muda mrefu ya watu kutokupenda kujiwekea akiba.

Amesema licha ya watu kutokuwa na tabia hiyo, hata vipato vya wengi ni vidogo.



Chanzo: mwananchi.co.tz