Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachumi: Bajeti inaingilia mikakati ya Serikali

Mwigulu Lkoo Bajeti inaingilia mikakati ya Serikali

Sun, 19 Jun 2022 Chanzo: Mwananchi

Licha ya maboresho kadhaa yaliyofanywa kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha, wachumi na wataalamu wa fedha wamesema kuna mambo yanahitaji kuwekwa sawa, ili kufanikisha malengo ya Serikali.

Maoni hayo yalitolewa jana jijini hapa kwenye mjadala wa bajeti ulioandaliwa na kampuni ya ukaguzi wa hesabu za fedha ya Ernst & Young na kuwashirikisha wataalamu kadhaa wa masuala ya uchumi na fedha.

Kati ya maeneo ambayo washiriki wa mkutano huo walisema yanajichanganya ni pale Serikali inaposisitiza kuhamasisha uchumi wa kidijitali, lakini inaweka kodi kwenye biashara zinazofanyika kielektroniki na tozo kwenye miamala ya simu.

Mkurugenzi mtendaji wa Ecobank, Mwanahiba Mzee alisema simu za mkononi zimechangia ujumuishaji wa wananchi kwenye huduma za fedha kwa kiasi kikubwa na zinawafaa wananchi wengi, hasa wa kipato cha chini.

“Kenya huwezi kufanya kitu bila Mpesa. Hata wauza mboga za majani wanataka uwalipe kwa Mpesa na wala hawaombi na ya kutolea, lakini hapa kwetu tumeongeza tozo juu.

“Hata hii Sh4,000 Serikali iangalie uwezekano wa kuiondoa, ili huduma hii iendelee kuwafaa watu wote. Sh4,000 inatosha nauli ya kumtoa mtu sehemu moja kwenda nyingine, kwa nini atumie huduma sasa?” alihoji Mwanahiba.

Advertisement Kuhusu tozo ya miamala, Mtafiti Mwandamizi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Samwel Wangwe alisema mpaka sasa kiasi kikubwa cha fedha iliyopo kwenye mzunguko ipo kwenye sekta isiyo rasmi na simu za mkononi ndilo jukwaa rahisi kwa wengi kuingia kwenye mfumo rasmi, lakini gharama zilizopo zinawakimbiza wengi.

“Matumizi ya fedha taslimu yanapunguza upatikanaji wa taarifa za kodi, hivyo ugumu wa kuikusanya. Simu zingerahisisha hili. Ila kwenye bajeti Serikali imesema inakusudia kuimarisha mifumo ya Tehama kukusanya mapato yake,” alisema Profesa Wangwe.

Mchumi huyo mwandamizi alisema Serikali ina vipaumbele vingi wakati kiasi kilichotengwa kwa ajili ya kulipa deni lake pamoja na mishahara ya watumishi ni takriban asilimia 70, hivyo kubakiza sehemu ndogo kwa ajili ya mambo mengine, ikiwamo miradi ya maendeleo.

“Kuwa na vipaumbele vingi kunaifanya bajeti isitekelezeke hivyo unahitajika mpango mahsusi kuangalia namna ya kuvipunguza kuendana na uhalisia, vinginevyo vitakuwa vinapangwa ila havitekelezwi,” alisema.

Sehemu nyingine yenye mkanganyiko ni jitihada za kuutangaza na kuufufua utalii ulioathiriwa kwa kiasi kikubwa na janga la Uviko-19, lakini Serikali imeweka Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye ndege za kukodi ambazo nyingi hutumiwa na wageni wanaotoka nje kwenda hifadhini.

Mtaalamu wa Kodi wa Kampuni ya Ernst & Young, Beatrice Melkiory alisema pendekezo la kutoza asilimia mbili kwenye biashara za mtandaoni zinazomilikiwa na watu kutoka nje kunatanua wigo wa kodi, lakini linapingana na mkakati wa kujenga uchumi wa kidijitali. “Hata mpango wa kutoza VAT kwa wanaokodi ndege ni kuingilia mipango ya kuutangaza utalii wa Tanzania kwa sababu wengi wanaozikodi ni wageni wanaoenda kuvitembelea vivutio vyetu,” alisema Beatrice.

Hata mamlaka yanayolengwa kupewa Waziri wa Fedha na Mipango kusamehe kodi kwenye miradi mikubwa ya uwekezaji, alisema utaratibu unatakiwa kuwa wa wazi zaidi, hasa muda utakaotumika kwa Baraza la Mawaziri na Kamati ya Uwekezaji Mkubwa kumruhusu waziri kutoa msamaha huo.

“Kwa watu wanaopinga makadirio ya kodi kwa sasa hawana uhakika wa kujibiwa. Sheria inatakiwa ieleze baada ya siku ngapi mlalamikaji atapata majibu ya rufaa aliyoikata. Hata huu utaratibu wa waziri kusamehe kodi kwenye uwekezaji, ielezwe utaratibu utakamilika ndani ya muda gani,” alisema Beatrice.

LHRC yataja mambo matatu

Baada ya Serikali kuwasilisha mapendekezo yake ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23 wiki hii, Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) kimetoa mapendekezo matatu kuiboresha.

Mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema suala la bima ya afya kwa wote linapaswa kutekelezwa sasa, kwani maoni yameshatolewa kilichobaki ni fungu lake tu.

“Baada ya kilio cha muda mrefu cha Watanzania wa kipato cha chini kukosa huduma za afya kwa kukosa fedha taslimu, bima ya afya ni mkombozi. Watendaji wamesikika wakizungumzia umuhimu wake, lakini kuna ukimya katika mapendekezo ya bajeti ya Serikali hata mwaka huu wa fedha,” alisema Anna.

Kituo hicho pia kimepinga kupunguzwa kwa kiasi cha mikopo ya halmashauri wanayopewa wanawake kutoka asilimia nne ya mwanzo mpaka asilimia mbili zinazopendekezwa kwenye bajeti ijayo.

Anna alisema LHRC inapendekeza kurudishwa kwa kiwango cha awali cha mikopo hiyo inayotolewa na halmashauri kwa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani.

Vilevile, Anna alizungumzia kuongezwa kwa ushuru wa forodha kwa baadhi ya bidhaa zitumiwazo na wanawake, yakiwamo mawigi kutoka asilimia 25 mpaka 35 na taulo za watoto (baby diapers) kutoka asilimia 25 hadi 35.

“LHRC inaona kuwa hii sio haki kwa watoto na wanawake ikizingatiwa kuwa uzalishaji wa ndani haukidhi mahitaji na ubora wake bado ni changamoto. Kijinsia, kupanda kwa ushuru wa forodha kwa taulo za watoto kunahatarisha afya ya ngozi ya mtoto,” alisema.

Wabunge nao

Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei ameshauri ununuzi wa ndege za abiria usitishwe kwanza badala yake inunuliwe ndege kubwa ya mizigo, kwani huu ndio wakati wake.

Dk Kimei alitoa kauli hiyo jana, alipochangia mjadala wa bajeti kuu ya Serikali akisema ni wakati wa kumshauri na kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan aridhie suala hilo. Mbunge huyo alitoa sababu za kutaka mpango huo kwamba unatokana na tahadhari za kiuchumi zilizopo duniani.

Alisema kutokana na hali ya uchumi wa dunia, huu si wakati wa kukopa kwenye masoko ya nje kwa kuwa riba zimepanda na inahitajika tathmini ya mara kwa mara ya viashiria vya kiuchumi katika utekelezaji wa bajeti iliyopendekezwa.

“Bajeti hii imetengenezwa kwenye mazingira magumu na ina vihatarishi vingi vya kiuchumi, lakini bajeti inabana sana kwa hiyo huu si wakati wa kukopa kwenye masoko ya nje kwa kuwa riba zimepanda,” alisema Dk Kimei. Mtaalamu huyo wa masuala ya benki na taasisi za fedha alipendekeza kama itafaa huu uwe wakati wa kupunguza baadhi ya miradi ya maendeleo, akitaja ununuzi wa ndege, licha ya kuwa ni jambo jema lakini linaweza kusubiri.

Kingine Dk Kimei aliipongeza Serikali kwa kuhamasisha matumizi ya bidhaa, hasa bia na soda kwa kutoongeza kodi akisema itasaidia kupunguza makali ya gharama za maisha.

Mbunge wa Hai, Saashisha Mafue aliiomba Serikali kuondoa ushuru kwenye ndege zinazotua na kuegesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) zinazokwenda kubeba mizigo.

Mafue alisema kitendo hicho kitasaidia kuongeza idadi ya ndege zitakazotua katika uwanja huo ambazo zinakwenda kubeba mbogamboga, jambo litakaloongeza na kukuza biashara ya mazao ya wakulima.

Chanzo: Mwananchi