Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachimbaji wadogo watakiwa kutumia vituo vya mfano

Wachimbaji Picbbb Vituo Wachimbaji wadogo watakiwa kutumia vituo vya mfano

Wed, 28 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu mkoani Geita wameshauriwa kutumia vituo vya mfano vya uchimbaji na uchenjuaji dhahabu vilivyopo mkoani hapa katika kujifunza namna bora ya kuchimba kwa teknolojia za kisasa bila kuathiri mazingira.

Akizungumza jana Septemba 27, 2022 katika uwanja wa EPZD yanakofanyika maonyesho ya tano ya teknolojia ya madini, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema Serikali ilianzisha vituo vya mfano vya Katente na Lwamgasa ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata ujuzi.

“Tunatarajia wachimbaji wadogo wapate ujuzi wa kufanya shughuli zao kuanzia utafiti, taarifa na namna ya kuchimba namna ya kutumia teknolojia za kisasa na namna ya kupata masoko ya bidhaa za madini,” amesema Mbibo.

Akizungumzia maonyesho ya teknolojia ya madini, Mbibo amesema maonyesho hayo ni fursa kwa wachimbaji wadogo kujifunza na kupata ujuzi wanamna bora ya kufanya shughuli zao kwa tija zaidi.

“Wakifika hapa wanaweza kujifunza watakutana na kampuni zinazoshiriki kwenye shughuli za madini tangu uchimbaji hadi uuzaji na pia vipo vyama vya wachimbaji, wakifika hapa wanaweza kuona ni namna gani ya kuunganisha nguvu kwa pamoja katika kukuza uchumi wao na wa nchi,” amesema Mbibo.

Kwa upande wake msimamizi wa kituo cha mfano cha kuchimba na kuchenjua dhahabu cha Lwamgasa, Victor Augustine amesema uwepo wa kituo hicho umewasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kwa usalama na njia bora zaidi tofauti na miaka ya nyuma.

Aidha kituo hicho pia kinawajengea uwezo wachimbaji wadogo kuchenjua kwa kutumia kemikali ya kaboni inayotumika kama mbadala wa zebaki ambayo ni hatari kwa usalama wa watu na mazingira.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo mkoani hapa (Gerema), Christopher Kadeo amesema kinachofanywa na Serikali sasa ni majibu ya kilio chao cha muda mrefu cha kutaka wachimbaji wawezeshwe na kupewa mbinu mbadala ya kuchimba kisasa.

“Sasa hivi tunajikwamua tumeanza kuachana na matumizi ya magogo, tunajua sio jambo rahisi lakini kidogokidogo mabadiliko yanaonekana kwa sasa yapo mashimo yanayojengwa kwa kutumia zege lakini mengine yanatumia vyuma kama winchi kunyanyua mizigo na inarahisisha kazi,” amesema Kadeo.

Maonyesho hayo yanayowakutanisha washiriki zaidi ya 600 kutoka ndani na na nje ya nchi wakiwemo kutoka China na India yameanza leo Septemba 27, 2022 na yanatarajiwa kufungwa Oktoba 8, 2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live