Licha ya wachimbaji wadogo wa dhahabu mkoani Geita kuzalisha kati ya kilo 400 hadi 500 za dhahabu kila mwezi, imeelezwa bado hawana utamaduni wa kuweka fedha zao benki na badala yake huzitunza kwenye mabegi jambo ambalo sio salama.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amewataka kuachana na utamaduni huo, badala yake watunze fedha zao benki mahali ambapo ni salama na penye fursa ya kupata mikopo bila usumbufu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi la benki ya biashara nchini (TCB) lililofunguliwa katika eneo la Soko la dhahabu mjini Geita Julai 31, 2023, Shigella amesema tawi hilo ni hatua muhimu katika kutekeleza mikakati ya kukuza uchumi wa mkoa huo.
“Huu mkoa ni miongoni mwa mikoa yenye mizunguko ya fedha kutokana na uzalishaji mkubwa wa dhahabu lakini bado wananchi wanaweka fedha ndani. Kufunguliwa kwa tawi hili kutaendelea kuhamasisha wananchi kuja benki kutunza fedha zao”amesema Shigella
Aidha amewataka wafanyabiashara na wajasiriamali waliopo kwenye mkoa huo kutoogopa kukopa kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya kukuza shughuli zao zitakazowasaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Ni matumaini kuwa benki hii itatatua changamoto za wananchi wa Geita na itaendelea kutoa elimu na fursa mbalimbali, nitoe wito kwa benki kutoa mikopo nafuu ili kuwafikia wafanyabiashara na kinamama ili waweze kujikwamua kiuchumi,”amesema Shigella
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya TCB, Sabasaba Moshingi amesema benki hiyo inatoa huduma mbalimbali za kifedha ikiwa ni pamoja na utunzaji wa amana, mikopo mbalimbali ya wafanyabiashara, wastaafu, vikundi pamoja na dirisha maalum la wanawake.
Amesema benki hiyo imekuwa na kufika nafasi ya tisa kwenye mizania kutoka kuwa benki ya huku, tawi la benki hiyo mkoani Geita likianza 2013 ambalo hadi sasa linawateja 5, 000 na tayari wametoa mikopo ya zaidi ya Sh9 bilioni kwa wananchi.
Ally Abdul mkazi wa mjini Geita amesema uwepo wa huduma za kifedha ni fursa kwa wananchi ambao watakopa na kufanya biashara lakini pia ni kiashiria cha kukua kwa shughuli za kiuchumi katika mkoa huo.