Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachimbaji wadogo wa madini wapewa mafunzo

48702 Madinipic

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mirerani. Wachimbaji wa madini wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamejengewa uwezo wa kuchimba madini kwa njia salama ili kuepuka ajali na vifo migodini.

Mhandisi wa migodi wa Tume ya Madini, Laurent Mayala akizungumza leo Jumanne Machi 26, 2019 amesema mafunzo kwa wachimbaji hao yanafanyika kwa siku mbili katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Mayala amesema sehemu za machimbo ni hatarishi kutokana na kufanya kazi zao chini ya migodi hivyo kupitia mafunzo hayo watachimba kwa usalama na kuepukana na ajali na vifo.

Amesema baadhi ya ajali huwa zinaepukika migodini ikiwemo ya ukosefu wa hewa hivyo kupitia mafunzo hayo wanatarajia hakutatokea ajali za namna hiyo.

"Sehemu hii kuna wachimbaji wengi hivyo kupitia mafunzo haya uchimbaji utakuwa na tija na kuepukana na ajali kwani thamani ya maisha ni kubwa kuliko madini wanayochimba," amesema Mayala.

Amesema wachimbaji hao wanaelezwa namna bora ya kuchoronga bila kudhuru afya kwa kupunguza vumbi ikiwemo kuepuka ugonjwa wa kifua kikuu.

Amesema wachimbaji hao wameelezwa kufahamu namna bora ya kufikisha hewa safi mgodini na utoaji udongo.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM katika kuboresha sekta ya uchimbaji madini.

Amewataka wachimbaji hao kuzingatia ipasavyo mafunzo hayo ili wayaboreshe ikiwemo utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti.

"Mnaweza kufika kwenye kampuni ya Tanzanite Africa ambayo ni mfano bora katika utunzaji wa mazingira migodini, mnapaswa kuiga hilo kwa kupanda miti mingi migodini," amesema.

Mwenyekiti wa Tanzanite, Money Yousuph amesema wachimbaji hao wanapaswa kupanda miti ambayo itaweza kustahimili mazingira ya migodini.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Shwaibu Mushi amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo zaidi wachimbaji hao katika shughuli zao za uchimbaji madini ya Tanzanite.

Mchimbaji wa madini ya Tanzanite, Rachel Njau amesema mafunzo hayo yanapaswa kufanyika mara kwa mara ili wachimbaji wakumbushwe wajibu wao kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za madini.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika mji mdogo wa Mirerani kwa kuhusisha washiriki 150 wakiwemo wamiliki wa migodi, mameneja, wachimbaji, madalali na wanaApolo.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz