WACHIMBAJI wadogo wa madini katika mkoa wa Mara wamechimba jumla ya tani 3.5 za dhahabu ndani ya kipindi cha miezi 12 mwaka 2019.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa mkoa huo, Ally Hapi kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara uliyofanyika mjini Musoma.
Alisema mwaka uliopita, mkoa huo ulishika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa madini Tanzania, ukikitanguliwa na mkoa wa Geita uliyoongoza katika uzalishaji wa maliasili hiyo.
Hapi alikuwa akiwasilisha taarifa ya serikali ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mihula miwili, yaani taarifa ya Mwaka 2019 na ya mwaka jana, ambazo zilikuwa hazijawasilishwa. Licha ya mafanikio aliyoyaelezea katika sekta ya madini mkoani humo, aliomba nguvu ya chama iongezwe ili serikali iweze kufanikiwa katika mipango yake ya kuongeza ufanisi na mapato kupitia ushimbaji rasilimali hizo.
Alisema kuna mpango wa kupanua Mgodi wa North Mara ambao unakwamishwa na baadhi ya wamiliki wa maeneo wanaotakiwa kupisha upanuzi huo.
“Sehemu baadhi wanaotakiwa kulipwa fidia wamekubali, lakini wengine wamekuwa wazito wakitaka fidia kubwa. “Serikali ina utaratibu wake katika kulipa fidia, hufanya tathmini kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwamo kuangalia vitu vilivyo kwenye ardhi husika kama vile mazao, nyumba na vinginevyo,” alisema.
Alisema fidia ya ardhi hulipwa kwa kuzingatia bei ya soko na kwamba madai yakiwa juu bei hiyo inaweza kusababisha mwekezaji kushindwa.
“Hilo likitokea, mgodi utacheleweshwa katika kutekeleza mpango yake na pengine mwekezaji akaachana nao na kuhamishia uwekezaji maeneo mengine ndani au nje ya mkoa huo,” alisema.
Alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Luteni Kanali Michael Mtenjele kuendelea kushughulikia changamoto hiyo huku wenye maeneo yanayoguswa na upanuzi huo akiwahakikishia hakuna ambaye hatalipwa lakini bei ya soko itazingatiwa.