Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachimbaji madini wawajibike kukabili mabadiliko tabianchi

Mud Matope Madini Wachimbaji madini wawajibike kukabili mabadiliko tabianchi

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Suala la mabadiliko ya tabianchi na athari zake hivi sasa linazungumzwa kama changamoto mpya ulimwenguni, nchi na mashirika mbalimbali yamekuwa yakibuni kila njia za kuzikabili.

Katika mkutano wa mwaka 2023 wa mabadiliko ya Tabia ya nchi Afrika uliofanyika jijini Nairobi, Kenya Rais Samia Suluhu Hassan alisema mabadiliko ya tabia ya nchi yameathiri uchumi wa watu katika mataifa mbalimbali.

Alishauri uzalishaji wa nguvu kazi yenye tija kwenye fursa ya biashara ya kaboni na kuuza nje bidhaa iliyokamilika badala ya malighafi ya madini ya kimkakati.

Kadhalika Rais Samia alitumia jukwaa hilo kushawishi viongozi wa Afrika kukubaliana kuzibana nchi za Ulaya zinazozalisha gesijoto duniani, kuchangia ufadhili katika mfuko maalumu ili kuiwezesha Afrika inayoendelea kuathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

"Tunapoelekea kwenye COP28, hatuna budi kuinuka kama sauti ya Afrika kuhusu uanzishwaji wa mfuko maalum kwa ajili ya Afrika. Wanapaswa kusema ni asilimia ngapi ya ahadi zao Afrika na sio vinginevyo,"alisema Rais Samia.

Wakati viongozi wa Afrika wakifikiria juu ya kuanzishwa wa mfuko wa mazingira, takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa shughuli za uziduaji wa rasilimali (Resource extraction) zinachangia nusu ya hewa yote ya kaboni inayozalishwa duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) katika baadhi ya maeneo uziduaji umechangia katika uchafuzi wa hewa, vyanzo vya maji, mmomonyoka wa ardhi na kutapakaa kwa taka zenye sumu katika mazingira.

Kutokana na hali ya mambo ilivyo wadau wa uziduaji na mazingira hapa nchini wameelezea nafasi ya kampuni za uchimbaji wa madini, mafuta na gesi katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza hali ilivyo hapa nchini Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Hakirasilimali Adam Antony alisema kuna haja ya kampuni za madini kuangalia namna sahihi ya kuendesha shughuli zao kwa namna inayopunguza athari zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi.

"Shughuli zinazohusisha uchimbaji wa madini, mafuta na gesi, zote zinachangia kwa kiasi fulani katika uzalishaji kaboni na hewa chafu zinazochangia mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Antony aliongeza kuwa kampuni zinazojihusisha na Sekta ya uziduaji kwa sasa ndio zimeanza kuangalia namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi japo sio kwa kiwango kinachotosha.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni uchimbaji wa madini yatumikayo kwa kiasi kikubwa kuchagiza matumizi ya nishati safi ambayo ni hatua muhimu ya kukabiliana na tishio la mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Mfano hapa kwetu tumeona wamewekeza katika uchimbaji wa madini ya kama kinywe, Nikeli na mengine yatakayotumika katika utengenezaji wa betri na sola ambazo zote ni malighafi zinazohitajika katika kupata nishati safi," alisema Adam.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Abel Kinyondo alisema ili kuzifanya kampuni za uchimbaji wa madini kuwajibika kwa uchafuzi wa mazingira inapaswa kutungwa sheria inayosimamia jambo hilo.

Alisema kwa sasa hakuna sheria inayolazimisha wala kusema wajibu wa kampuni hizo katika ufadhili wa hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

“Hali ilivyo sasa jambo hilo ni la utashi sio la lazima lakini kulingana na unyeti wa suala na mabadiliko ya tabianchi matamanio ni kuwa mkazo wa kisheria wa jambo hilo. Ukiwauliza wachimbaji sasa hivi watakwambia wanalipia gharama hizo kupitia kodi lakini uhalisia ni kwamba fedha hizo zinawekwa kwenye kapu la jumla huwezi kuzitenganisha,” alisema Kinyondo.

Alishauri kuwa ni muhimu kuwa na utaratibu wa ‘carbon pricing au carbon trading’ (utaratibu wa wazilishaji wakubwa wa kaboni kuwalipa au kugharimia miradi ya utunzaji wa mazingira).

“Kwa mtindo huo watalipa kiasi stahiki kwa ajili ya kutunza mazingira, Kimsingi watalipa zaidi kwakuwa wao ni wachafuzi wa mazingira wakubwa na watunza mazingira watapata manufaa kwa juhudi muhimu wanazozifanya,” alisema Profesa Kinyondo.

Kaimu meneja wa kitengo cha uwazi na uwajibikaji wa Taasisi ya uhamasishaji uwazi na uwajibikaji (TEITI), Joseph Kumburu alisema kampuni nyingi za uziduaji zinachangia kwenye kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema Kumburu na kuongeza kuwa Baraza la Taifa la uhifadhi wa mazingira (NEMC) linasimamia vyema hivyo, hata TEITI imeanza kujumuisha taarifa za masuala ya mazingira katika ripoti zao.

Hata hivyo Ofisa Uchechemuzi (advocacy) na mahusiano kutoka shirika la Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT), Awadhi Rashid alieleza namna makampuni yanayojihusisha na uziduaji yanavyochangia kwenye mabadiliko ya tabia ya nchi kuliko kuzuia.

“Magari na mashine zinazotumika huko migodini nyingi zinatumia mafuta tena kwa wingi hali inayoongeza uzalishaji wa hewa chafu ambayo ina athari katika mazingira.

“Binafsi naona wanaharibu zaidi mazingira kuliko watunzavyo"

Katika siku za hivi karibuni Waziri wa fedha Dk Mwigulu Nchemba amenukuliwa mara kadhaa akieleza namna ambavyo mabadiliko ya tabia ya nchi yalivyochangia kuzorotesha ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Wakati wa mkutano wa Serikali na washirika wa maendeleo mapema mwaka huu Dk Nchemba alisema mabadiliko ya tabia yametoa somo kwa Tanzania namna inavyopaswa kujipanga katika kilimo cha umwagiliaji kwakuwa misimu ya mvua imekuwa haitabiriki jambo ambalo linaathiri kilimo cha kutegemea mvua.

Oktoba 2022 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk Selemani Jafo alisema takribani Dola za Marekani bilioni 19.2 (Sh47.9 trilioni) zitatumika katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko Tabianchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live